CCM haitishwi na wingi wa wagombea

CHAMA Cha Mapinduzi Zanzibar kimesema hakitishwi wala kubabaishwa na wingi wa wagombea wa vyama vya siasa wanaojitokeza kuchukua fomu za urais wa Zanzibar kwani hiyo ndiyo demokrasia ya mfumo wa vyama vingi.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Kisiwandui mjini hapa, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Vuai Ali Vuai alisema vyama vya siasa vitapimwa kutokana na uwezo wake wa kusimamia na kutekeleza ilani ya uchaguzi iliyojiwekea.
Alisema Chama Cha Mapinduzi kinajivunia na utekelezaji uliotukuka wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010- 2015 ambayo imefanikiwa kwa asilimia 90 katika maeneo yote muhimu ikiwemo ustawi wa jamii, uchumi na sekta ya kilimo.
“ Napenda kuweka bayana kwamba Chama Cha Mapinduzi hakibabaishwi wala kutishika na utitiri wa wagombea wa vyama vya siasa walioibuka katika kinyang'anyiro cha kuchukua fomu kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba 25......chama cha siasa kitapimwa na uwezo wake wa kusimamia na kutekeleza ilani ya uchaguzi wake,” alisema.
Katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar tayari jumla ya vyama 15 vimejitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar ikiwa hiyo ni mara ya kwanza kuwepo kwa idadi kubwa ya vyama vya siasa.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved