Watakaouza nguzo za umeme kufukuzwa


SERIKALI imesema itawafukuza makandarasi watakaobainika kuuza nguzo za umeme. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alitoka kauli hiyo jana bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM).
Ndassa alitaka kujua kwa nini wananchi wamekuwa wakiuziwa nguzo moja ya kuunganishia umeme kwa Sh 300,000 na kwa nini kumekuwa na ucheleweshwaji wa miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kwani mingi haitekelezwi kwa wakati.
Akijibu swali hilo Profesa Muhongo alisema, serikali itawafukuza makandarasi wote watakaobainika kuuza nguzo za umeme. Alisema endapo mkandarasi ataonekana kukiuka utaratibu adhabu yake ni kutopata mradi wa REA kuanzia mwaka huu.
Alisema miradi mingi ikiwemo ya REA ilishindwa kuendelea kama ilivyopangwa kutokana na fedha nyingi kuelekezwa kwenye uchaguzi mkuu na Bunge la Katiba. “Sasa Serikali itamalizia miradi mikubwa na fedha zinakwenda REA, miradi itakamilika kama ilivyopangwa,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Maryam Msabaha (Chadema) katika swali la nyongeza alitaka kujua sababu za serikali kurundika nguzo hasa maeneo ya vijijini kwa muda mrefu hali inayofanya nguzo nyingi kuoza. Akijibu swali hilo, Profesa Muhongo alisema, nguzo huwa haziozi hata kama zimerundikwa kwa miaka 10.
Pia alisema Tanzania ina vijiji 15,029 ambapo vijiji 5,900 sawa na asilimia 33, vimeunganishwa na umeme wa REA. Alisema ikiingia REA awamu ya tatu, nne na tano Tanzania itakuwa nchi ambayo vijiji vyake vingi vina umeme katika Afrika.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved