JK: Sifa yangu ni kutekeleza ahadi.

  HUKU akikaribia kukabidhi madaraka kwa Rais wa Awamu ya Tano baadaye mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete amesema moja ya sifa yake na ya chama tawala, CCM, ni kutekeleza ahadi walizowaahidi Watanzania wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010.
Amesema ahadi nyingi alizowaahidi wananchi ambazo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, zimetekelezwa. Aidha, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alisema utawala wa Rais Kikwete umekuwa na mafanikio makubwa kwenye sekta ya ujenzi.
Amesema katika kipindi cha miaka 10, serikali imenunua vivuko vipya 15 na kukarabati vivuko saba na kwamba hayo yote yamefanikiwa kwa kuwa Watanzania walimuamini Rais Kikwete na kumpa nafasi ya kutekeleza ahadi kwa vitendo. Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akizindua kivuko cha Mv Mafanikio kinachofanya safari zake kati ya Mtwara na Msangamkuu.
Alisema wakati wa kampeni mwaka 2010, aliwaahidi wananchi wa Msangamkuu kuwapatia kivuko ambapo ahadi hiyo imetekelezwa. “Hiyo ndio sifa yangu pamoja na chama chetu, tunapoahidi tunatekeleza kwa vitendo na leo hii wananchi wa Msangamkuu wameondokewa na kero ya usafiri waliokuwa wanapata,” alisema.
Alisema kivuko hicho ni fursa nzuri kwa kukuza uchumi wa wananchi na amewataka waitumie vizuri fursa hiyo. Rais Kikwete alisema wananchi wa Msangamkuu walikuwa wanapata shida ya usafiri na kwamba walikuwa wanalazimika kuzunguka umbali wa kilomita 21 hadi kufika Mtwara mjini, hivyo adha hiyo kwa sasa itakuwa historia.
Kwa upande wake, Dk Magufuli alisema katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wa Rais Kikwete amefanikiwa kununua vivuko vipya 15 na kukarabati saba ambavyo hivi sasa vinafanya kazi kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Alisema tangu serikali ya awamu ya kwanza mpaka serikali ya awamu ya tatu, kulikuwa na vivuko 13 na kwamba hivi sasa vipo zaidi ya 28. “Hatuna budi kukushukuru Mheshimiwa Rais kwa kuboresha huduma mbalimbali za usafiri, utawala wako umeweza kununua vivuko vipya 15 na kukarabati saba hilo si jambo dogo, tunakushukuru sana na rais ajae ataendeleza zaidi ya hapo ulipoishia,” alisema huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliojitokeza.
Alisema kivuko hicho kimegharimu Sh bilioni 3.3, ambazo zimetolewa na serikali. Dk Magufuli ambaye ni mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, alisema wanafunzi na walemavu watavuka bure katika kivuko hicho na kwamba watu wazima watalipia Sh 300, watoto Sh 100.
Dk Magufuli alisema Rais Kikwete aliahidi barabara kutoka Dar es Salaam mpaka Mtwara ambayo hivi sasa imekamilika. “Watanzania wana kila sababu ya kukushukuru Rais Kikwete umewafanyia mambo mengi, wewe ni kiongozi mwenye upendo, imani na kubwa zaidi umetekeleza kwa vitendo uliyoahidi,” alisema.
Aidha alitumia fursa hiyo kujitambulisha kwa wananchi waliojitokeza kwa wingi kuwa ndiye mgombea urais wa CCM. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Marcelin Magessa, alisema mkoa wa Mtwara kuna vivuko viwili kikiwemo cha Mv Kilambo na Mv Mafanikio.
Alisema kivuko cha Mv Mafanikio kilitengenezwa na mkandarasi wa hapa nchini na kwamba kilianza kutoa huduma mwaka jana. Alisema kivuko hicho kina uwezo wa kubeba abiria 100, tani 50 na magari matatu kwa wakati mmoja.
Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia, alisema wananchi walikuwa wakipata shida ya usafi ambapo baadhi yao walipoteza maisha kutokana na kukosa usafiri wa uhakika. Alisema ujenzi wa kivuko hicho unatokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Dk Magufuli na kwamba wananchi wa jimbo hilo wanampongeza.
Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu, alisema kata ya Msangamkuu ina wakazi zaidi ya 1,200, ambapo kivuko hicho ni mkombozi mkubwa kwa wakazi hao. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mussa Iyombe, wabunge na wananchi ambao walijitokeza kwa wingi.

Lowassa awapoza CUF kuondoka kwa Lipumba

  MGOMBEA urais wa Chadema anayeungwa mkono na vyama vingine vitatu vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa amewapa pole wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa mshituko wa kuondokewa na Mwenyekiti wao wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu, huku akiwataka kutovunjika moyo, bali waongeze mshikamano ili dhamira ya kuingia Ikulu iweze kutimia.
Aidha, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe ameonya kuwa, hawatamvumilia yeyote atakayeonekana kutaka kukwamisha umoja wao unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Akizungumza na wananchi waliofika kumpokea alipotembelea ofisi za CUF Buguruni, Dar es Salaam jana ambako pia alihudhuria kikao cha Baraza Kuu la CUF, Lowassa aliwapa pole wanaCUF akisema endapo watatetereka, safari yao ya kuelekea Ikulu itakuwa ngumu.
Alitumia fursa hiyo kuwaomba wafuasi wa CUF kumsindikiza kwa wingi leo kwenda ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu ya kuwania urais baadaye mwaka huu, huku akisisitiza ana imani ya kushinda.
Awali, mgombea mwenza wa Lowassa, Juma Duni Haji ambaye alijiunga Chadema hivi karibuni akitokea CUF alikokuwa Makamu wa Mwenyekiti wa Taifa, alisema endapo wanachama wa vyama vinavyounda Ukawa watakosea katika kupiga kura zao na kushindwa kuingia madarakani, basi watalazimika kusubiri miaka 50 ijayo ili kuingia Ikulu.
“Tusipoweza kuingia Ikulu sasa litakuwa kosa kubwa na itatulazimu kusubiri miaka 50 ijayo ili kuweza kuchukua madaraka. Vijana pekee ndio watakaoweza kuleta mabadiliko,” alisema Duni.
Akizungumzia shughuli ya kuchukua fomu leo, Lowassa aliwataka wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kumsindikiza na kusisitiza kuwa amejiunga na Ukawa ili kutafuta mabadiliko nje ya CCM na kuwa ana imani ya kushinda kwa asilimia 90.
Lowassa alisema endapo Ukawa itashinda na kuchukua madaraka wataendesha nchi kwa utulivu na kubadilisha maisha ya Watanzania kwa kuwaondolea umasikini ambao umekuwa ukipigwa vita tangu mwaka 1962. Naye Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alisema kiongozi ndani ya Ukawa ambaye atakuwa akipingana na malengo yao kutokana na kukosa fursa binafsi, mtu huyo hafai kuwa katika umoja huo.
Alisema pamoja na umoja huo kukumbwa na misukosuko, bado wamekuwa wamoja na kutetea hatua ya wao kumteua Lowassa ambaye wiki mbili zilizopita alikuwa CCM kwa sababu ni Mtanzania. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema silaha pekee ya ushindi kwa Ukawa ni kuwa na umoja, ushirikiano na mshikamano na kuwa ana uhakika Lowassa atashinda, sambamba na yeye kwa upande wa Zanzibar.
“Lowassa ni rais anayesubiriwa kuapishwa, na Zanzibar kuna mtu anaitwa Maalim Seif ameshamaliza kazi naye anasubiri kuapishwa,” alisema na kuongeza kuwa amefarijika kwa Lowassa kutembelea CUF, jambo ambalo linadhihirisha umoja wao.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia alisema Ukawa haitahubiri siasa za chuki ili uchaguzi ufanyike kwa amani na kuwaonya viongozi wa CCM kuchunga ndimi zao. Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema watakaoiondoa CCM madarakani ni wananchi wenyewe kwa kujitokeza kupiga kura.
Lowassa leo atachukua fomu ya uteuzi wa urais katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), akiambatana na mgombea mwenza Duni. Msafara wa kumsindikiza Lowassa, utaanzia Makao Makuu ya CUF, Buguruni asubuhi saa 2:00 na kupitia Makao Makuu ya NCCRMageuzi na baadaye kwenda NEC ambapo saa 5:00 asubuhi mgombea huyo atachukua fomu.
Baada ya kuchukua fomu, Lowassa ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu kwa kashfa ya kuiingiza Serikali katika mkataba wa kufua umeme wa kampuni feki ya Richmond na baadaye kuchujwa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia CCM, atakwenda Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni.
Wakati huohuo, Emmanuel Ghula anaripoti kuwa Chama cha Wananchi (CUF) kimechagua kamati ya watu watatu ambao watafanya kazi zilizokuwa zikifanywa na Mwenyekiti wa chama hicho aliyejiuzulu, Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na makamu wake, Juma Duni Haji.
Walioteuliwa ni Twaha Taslima ambaye atakuwa mwenyekiti wa kamati, Abubakar Khamis na Severina Mwijage. Kuundwa kwa kamati hiyo kunatokana na kujiuzulu kwa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Lipumba huku makamu mwenyekiti wake kujiunga na Chadema kama mgombea mwenza wa urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akitangaza uamuzi wa baraza kuu la uongozi wa taifa wa chama hicho, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema kuwa chama hakiwezi kukaa kwa kipindi cha miezi sita bila kuwa na mwenyekiti wala makamu wake, wameamua kuteua kamati ya watu watatu kama ambavyo katiba yao inawataka.
“Kwa mujibu wa katiba ya chama chetu, hatuwezi kuteua mwenyekiti wala makamu wake hadi kipindi cha miezi sita na badala yake katiba inaturuhusu kuteua kamati ya watu watatu watakaofanya kazi ambazo zilikuwa zinafanywa na viongozi hao wa juu,” alisema Maalim Seif.

Mbunge wa Viti Maalum CUF, Clara Mwatuka afariki kwa ajali.

mwatuka
Clara Mwatuka enzi za uhai wake.
Aliyekuwa Mbunge wa Viti maalumu kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Clara Mwatuka, amefariki dunia leo Jumapili jioni baada ya gari lake alilokuwa akisafiria kupinduka lilipokuwa linashuka eneo la Makonde Plateu kuelekea Ndanda, Masasi mkoani Mtwara.
mwatuka gari
Gari alilopata nalo ajali marehemu Mwatuka.

Gari ilikuwa inaendeshwa na dereva wake, ambaye inasemekana ni mwanaye. Maiti ya marehemum Mwatuka imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Ndanda.
Viongozi waandamizi wa CUF wamethibitisha kutokea msiba huo.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. AMEN.

Ratiba ya LOWASA wiki ijayo,unaweza kuipitia hapa..

Simba yatakata Taifa

  SIMBA ya Tanzania jana ilisherehekea vizuri siku yao (Simba Day), baada ya kuifunga Club Sports Villa ya Uganda 1-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo ulikuwa mahsusi wa kuhitimisha wiki ya Simba Day, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Singida Mjini anayemaliza muda wake, Mohamed Dewji.
Dewji hivi karibuni alitangaza kutogombea kiti hicho tena. Ushindi huo ni mwanzo mzuri kwa kocha Muingereza Dylan Kerr ambaye hivi karibuni alilalamikia ubutu wa safu yake ya ushambuliaji timu hiyo ilipokuwa kambini Zanzibar, ambako ilicheza mechi kadhaa za kirafiki.
Bao hilo pekee lilifungwa na Awadhi Juma katika dakika ya 90 ya mchezo huo baada ya kutokea piganikupige langoni mwa Club Sports Villa.
Simba iliuanza mchezo huo kwa kasi lakini jitihada zao za kusaka bao zinakwamishwa na Hamisi Kiiza ambaye alishindwa kufunga bao la kuongoza katika dakika ya 13 baada ya kupata nafasi nzuri lakini akachelewa kufanya maamuzi na beki wa Club Sports Villa, Mbowa Paul akauokoa.
Villa wanajibu mapigo katika dakika ya 17 wakati Achema Robert anakuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, lakini anapaisha mpira nje ya lango. Dakika ya 23 Simba iliendelea kukosa mabao wakati Mussa Mgosi akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga, alipiga mpira nje. Dakika mbili baadaye, Kiiza alipata mpira lakini kabla ya kulifia lango, mpira huo unazuiwa na beki mmoja wa Villa.
Villa ilipata pigo baada ya mchezaji wao, Waibu Yeseni kutolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumchezea Ibrahim Ajibu.
Dakika ya 55 Simba walikosa tena bao wakati Mgosi alipiga shuti lililodakwa kirahisi na kipa wa Club Sports Villa, Odongo Steven, huku Mohamed Hussein akipiga shuti nje ya 18 na kutoka nje ya lango.
Kikosi Simba: Vicent Angban, Ramadhani Kessy/Emiry Nimuboma, Mohamed Hussein, Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Justuce Majbva/Haji Nuhu, Said Ndemla, Ibrahim ajibu/ Mwinyi Kazimoto,Hamisi Kiiza, Mussa Mgosi na Peter Mwalyanzi/Simon Sserunkuma.
Aidha; Katika mchezo wa utangulizi ambao uliwahusisha viongozi wa Simba na wasanii, Simba ilitamba kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja huohuo huku bao hilo pekee likiwekwa kimiani na kocha wa timu hiyo, Kerr.

Pinda avunja ukimya alivyokatwa Dodoma

  WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amesema hawezi kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwataka waliohama baada ya kubwagwa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea urais, kujiuliza iwapo wataihama nchi wakishindwa kufanikisha malengo yao huko walikohamia.
Pinda alisema hayo jana alipohutubia wakazi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, alipokuwa akifunga maonesho ya wakulima ya Nanenane kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Alisema wakati wa mchakato wa kura za maoni, kila mmoja alipokuwa akizunguka mikoani kusaka wadhamini, alikuwa akiamini yeye ndiye anayeweza kupita, lakini hatimaye wachache walivuka hatua ya kwanza na wengine kuachwa nje na hatimaye mwisho akapatikana mmoja anayefaa zaidi.
Alisema haikuwa kosa kwa mmoja kati ya wagombea 38 waliorejesha fomu kupewa nafasi hiyo, kwa kuwa chama kiliamini anafaa na hivyo kinachopaswa kufanyika na makada wengine, ni kuendeleza chama ili kishinde kwa kishindo.
“Tulijitokeza wengi kuchukua fomu, watatu wakashindwa kurejesha fomu, wakawa wamejitoa wenyewe. Tulibaki thelathini na nane tuliorejesha fomu na kati ya hao wapo waliopita na wengine wakawekwa pembeni. “Mimi pia nikawekwa pembeni. Ninaamini kazi tuliyokwenda kuifanya tumeifanya vizuri, tena vizuri sana. “Sasa hapa katikati nilikaa kimya kidogo, watu wakaanza kusema kwenye mitandao… Oooh mbona mzee kimya! Au naye anataka kuhamia kule. Sasa niseme nimeachwa huku kwa hiyo nifanyaje? Nihame niende wapi? Hivi ukihama huku huko unakohamia ukishindwa utahamia wapi tena? Au ndiyo utahama nchi? “Wana uhakika gani na huko wanakohamia? Mbona nako kila siku tunasikia ya kusikia. Mivutano haiishi. Kila siku tunaona mambo. Tutabanana hapahapa, kama ni kusahihishana tutasahihishana humu humu,” alisema.
Hahami
Alisema hana mpango wowote wa kuacha chama hicho kwa kuwa amekulia humo na manufaa mengi ameyapata kupitia chama hicho, ikiwemo madaraka ya uwaziri mkuu kwa miaka nane.
Pinda alisema hataki kuwa miongoni mwa makada wachache wa chama hicho waliohama na kusahau mema waliyofanyiwa, huku akisema watu hao wametimiza usemi wa ‘Asiyeshukuru ni Kafiri’.
Aliwataka Watanzania kutodanganyika na viongozi wachache wenye uchu wa madaraka, wanaoshawishi kutokubaliana na mambo mazuri yanayofanywa na Serikali na badala yake wajiulize ni akina nani hao wanaotaka kuvuruga Taifa?
Waziri Mkuu alisema CCM ina Ilani yenye sera nzuri, na ndicho chama kinachopaswa kuaminiwa na Watanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao na kuthibitisha kuwa anayo imani na sera ya CCM, hana mashaka kuwa chama hicho kitapata ushindi mnono kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Waziri Mkuu huyo alipongeza jitihada zinazofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC) katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, ikiwemo uandikishaji wapigakura ambao wamevuka malengo yaliyowekwa awali.
Alisema licha ya changamoto nyingi zilizoibuka tangu kuanza kwa uandikishaji wapiga kura nchini kupitia mashine za Biometric Voters Register (BVR), Tume imeandikisha zaidi ya wapiga kura milioni 24 na imevuka malengo yaliyowekwa awali.
*Nyuki wavamia
Katika hatua nyingine, nusura shughuli ya kufunga maonesho ya wakulima ya Nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ndani ya viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, iharibike baada ya kutokea kwa kundi la nyuki waliovamia katika uwanja huo.
Nyuki hao walivamia eneo la Banda Kuu la mikutano ndani ya viwanja vya John Mwakangale, wakati shamrashamra za kufunga maonesho hayo zikiendelea.
Nyuki hao waliokuwa wakisafiri, walifika sehemu hiyo wakitokea upande wa Kusini Mashariki mwa Uwanja na baada ya kufika hapo umati wa wananchi ulipata wakati mgumu kwani wapo baadhi ya watu ambao walianza kuhaha kwa kulala chini, huku wengine wakibaki wameduwaa wasijue la kufanya.
Waandishi wa habari waliokuwa mashariki mwa jukwaa kuu, ni miongoni mwa watu waliolazimika kuinama kwenye kichumba kidogo kusubiri kwa muda mpaka nyuki hao walipoondoka.
Baada ya nyuki hao kupita, mwongozaji wa shughuli hiyo, Charles Mwakipesile alimtania Pinda kuwa nyuki hao walipita kumsabahi rafiki yao, kwa kuwa wanatambua kuwa amekuwa mstari wa mbele kupigania maisha yao kutokana na faida kubwa walizo nazo kwa binadamu.

Mh, Dkt. John Pombe Magufuli leo ndani ya mbeya..

Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli leo  tarehe 7 aug 2015 anatarajiwa kuingia ndani ya mkoa wa mbeya kwa ajili ya kuzungumza na wananchi, na wanachama wake..
Kaa Nasi New Day Taarifa Kwaajili ya taarifa zote na vitu vyote vitakavyo jili hivi punde..

Mkwasa atangaza 29 Stars

Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Charles Boniface Mkwasa leo ametangaza kikosi cha wachezaji 29 watakaongia kambini siku ya Jumapili tarehe 9, Agosti katika hoteli ya Tansoma iliyopoe eneo la Gerezani kwa ajili ya kambi ya wiki moja ya mazoezi.
Katika kikosi hicho alichokitangaza cha wachezaji 29, Mkwasa amewajumuisha wachezaji watano wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi (Proffesional), ambao baadae watajumuika kwa kambi ya kujiandaa kucheza na Nigeria mwezi Septemba 2015 nchini Uturuki.
Taifa Stars inatarajiwa kuweka kambi ya siku kumi jijini Istambul – Uturuki, ambapo itacheza michezo miwili ya kirafiki na timu za Taifa za Libya na Kuwait kabla ya kurejea nchini kuwavaa Nigeria.
Wachezaji watakaongia kambini jumapili ni magolikipa, Ally Mustafa (Yanga SC) na Aishi Manula (Azam FC), walinzi wa pembeni: Shomari Kapombe (Azam FC), Michael Aidan (Ruvu Shooting), Juma Abdul, Mwinyi Haji (Yanga SC) na Abdi Banda (Simba SC).
Walinzi wa kati; Hassan Isihaka (Simba SC), Nadir Haroub, Kelvin Yondani (Yanga SC), Viungo wakabaji: Himid Mao, Frank Domayo, Mudathir Yahya (Azam FC), Viungo washambuliaji ni Salum Telela (Yanga SC) na Said Ndemla (Simba SC).
Washambuliaji wa pembeni; Orgenes Mollel (Aspire – Senegal), Abdrahman Mbambi (Mafunzo), Deus Kaseke, Saimon Msuva (Yanga SC), Ramdhani Singano, Farid Musa (Azam FC), huku washambuliaji wa kati wakiwa ni John Bocco, Ame Ally (Azam FC) na Rashid Mandawa (Mwadui FC).
Wachezaji wa kimataifa waliojumuishwa katika kikosi hicho ambacho Agosti 23 kitaelekea kambini nchini Uturuki kwa kambi ya siku kumi ni Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu (TP Mazembe – DR Congo), Mrisho Ngasa (Free State – Afrika Kusini) na Hassan Sembi (Santos FC – Afrika Kusini) na Adi Yussuf (Mansfield Town – Uingereza)

Lipumba aipasua kichwa CUF

  WANACHAMA wa Chama cha Wananchi (CUF) jana walimbana Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba wakimtaka kueleza ukweli juu ya taarifa zinazodai kuwa amejiuzulu wadhifa huo.
Wanachama hao walifika asubuhi na kukusanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya CUF Buguruni, Dar es Salaam, kwa lengo la kujua hatma ya kiongozi wao huyo. Walipofika hapo, alikuwa na kikao kirefu na wazee na viongozi wa dini kuhusu kile alichotaka kukieleza mbele ya vyombo vya habari. Baada ya kuwepo kwa kelele nyingi na za muda mrefu, zilizokuwa zikipigwa na wanachama hao zaidi ya 200, waliokuwa wakiimba nyimbo mbalimbali, ilimlazimu Profesa Lipumba kutoka ofisini kwake na kuwatuliza.
Hata hivyo, wanachama hao waliendelea kubaki na sintofahamu kutokana na yale aliyowaambia. Lipumba aliwataka wanachama hao, kuielewa vizuri Katiba ya CUF, kwa kuwa chama hicho kinaendeshwa kwa kufuata Katiba. Alieleza kuwa kila mwanachama kwa nafasi yake, anatakiwa kukijenga chama hicho.
“Mwaka 1995 nilikuwa ni mwanachama wa kawaida na niliteuliwa kuwa mgombea urais. Chama chetu ni taasisi, tena kubwa na sio mtu mmoja, hivyo tujenge chama chetu kama taasisi,” alisema Profesa Lipumba kisha kurudi ofisini kwake.
Hata hivyo, wanachama hao waliendelea kupiga kelele za kutaka ufafanuzi wa kauli hiyo, ambayo wengi walidai kuwa haijaeleweka inamaanisha nini. Mmoja wa viongozi wa dini, aliyejitambulisha kuwa ni Mchungaji Godfrey Sombi alisema hali si shwari, kwani Profesa Lipumba anataka kubaki mwanachama wa kawaida ndani ya chama hicho.
Mchungaji Sombi alisema sababu kubwa ni kutokana na baadhi ya viongozi wa Umoja wa vyama vinne vya upinzani (Ukawa), ambao chama hicho ni miongoni mwa vinavyounda umoja huo, kuvunja malengo yake.
“Hajaridhishwa na ujio wa Lowassa (Edward) ndani ya Ukawa na kupewa nafasi ya kupeperusha bendera kwa nafasi ya urais, kwa hiyo anataka kubaki kuwa mwanachama wa kawaida,” alisema kiongozi huyo wa dini.
Lowassa amejiunga na Ukawa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wiki moja iliyopita na juzi aliteuliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho na umoja huo, wenye vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanachama wa CUF walimtaka Profesa Lipumba kuweka wazi kuhusu taarifa zinaripotiwa na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Walitaka Profesa huyo maarufu wa Uchumi na aliyegombea urais mara nne tangu mwaka 1995, aendelee kuwa kiongozi wao, kwani wana imani naye. Abdallah Simba alisema kauli iliyotolewa na Profesa Lipumba, bado imewafumba macho, kwani hawaelewi ukweli wa taarifa za kujiuzulu na walitegemea angetoa taarifa za kukanusha kujiuzulu ndani ya chama hicho au kueleza kinachoendelea.
Kwa upande wake, Hamis Issa alisema wao kama wanachama, hawataki suala la kujiuzulu kwa Profesa Lipumba litokee, kwani wanaamini ni kiongozi mwenye uwezo mkubwa anayeweza kuwafikisha mbali zaidi.
Awali, Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya alisema mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Profesa Lipumba, umeahirishwa mpaka siku nyingine kutokana na mwenyekiti wao kuwa na kikao na wazee na viongozi wa dini.
“Mwenyekiti ndiyo aliwaita alitaka kuzungumza na ninyi yaliyo moyoni mwake, lakini asubuhi amevamiwa na wazee na wanachama katika ofisi yake, wazee wanataka kujua yanayoendelea.
Hata mimi mwenyewe sijui alikuwa anataka kuzungumza nini ndio kuna hicho kikao wazee wanataka kujua alikuwa anataka kusema nini na vyombo vya habari,” alisema Sakaya.
Wakati wote wakati kikao kati ya Profesa Lipumba na wazee kikiendelea, wanachama hao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za chama na kumsifu huku wakitaka aje kuzungumza nao.
Wakati Profesa Lipumba akiondoka katika ofisi hizo, wanachama hao walitaka gari lake ambalo wakati huo halikuwa na bendera ya chama hicho kikuu cha zamani cha upinzani nchini, liwekwe bendera kuashiria ni gari la kiongozi wa chama.
Tangu Lowassa aruhusiwe kujiunga na Ukawa na baadaye Chadema, kumeibuka mgawanyiko ndani ya Chadema na sasa CUF, baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kujiweka kando akipinga Waziri Mkuu huyo wa zamani waliyemtangaza kwa miaka saba kuwa fisadi, kujiunga nao na kuwa mgombea urais.
Profesa Lipumba alikuwapo wakati Ukawa ikitangaza kumkaribisha katika umoja wao, na pia wakati Chadema ikimtangaza kuwa mwanachama wao. Lakini, baadaye alianza kukosekana katika matukio muhimu ya umoja huo.
Juzi hakuwapo wakati Lowassa akipitishwa na Mkutano Mkuu wa Chadema kuwa mgombea urais pamoja na Mgombea Mwenza, Juma Duni Haji ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF Zanzibar na sasa amehamia Chadema.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad alihudhuria mkutano huo, uliofanyika Dar es Salaam na alitangazwa kuwa Mgombea wa Urais wa Ukawa kwa Zanzibar.

BREAKING NEWS: Profesa Lipumba ajiuzulu rasmi Uenyekiti CUF

  MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amejiuzulu rasmi wadhifa wake huo ndani ya chama kwa kikle alichokitaja kuwa ni kukiukwa kwa Katiba ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba amesema UKAWA ilianzishwa kwa lengo la kusimamia rasimu ya katiba mpya kutokana na maoni ya wananchi "sasa wenzetu wamegeuza UKAWA kwa kuleta mtu ambaye alishiriki kupitisha katiba pendekezwa ambayo siyo maoni ya wananchi hivyo kiongozi atakayeshinda kupitia UKAWA hawezi kusimania maoni ya wananchi ya rasinu iliyopendekezwa na Warioba," amesema Lipumba.
Cha ajabu ni kwamba wakati wa vikao vya kumpitisha Lowassa kuwa mgombea wa Ukawa, Profesa Lipumba alikuwepo na ndiye aliyetoa taarifa kuhusu ujio wa Lowassa, hivyo taarifa hii inakinzana na kile alichokisema hapo awali. Kujiuzulu huko kunahitimisha wasiwasi wa muda sasa ndani ya chama chake kuhusu hatima yake kutokana na sababu ambazo hazikujulikana mara moja.
Profesa Lipumba alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama mwaka 1999 na kugombea urais katika vipindi viinne ambavyo vyote alishindwa.
Tutawaletea habari kamili hivi punde.

Yanga wamuuza Sherman

  KLABU ya soka ya Yanga imefanikiwa kumuuza kwa mkataba wa miaka mitatu mshambuliaji wake raia wa Liberia, Kpah Sherman aliyejiunga na timu ya Mpumalanga Black Aces iliyopanda kucheza Ligi Kuu ya Afrika Kusini ya PSL msimu huu.
Sherman alilazimika kuondoka nchini wiki iliyopita na kuiacha timu yake Yanga ikiwa kwenye michuano ya Kombe la Kagame kwa ajili ya kukamilisha vipimo vya afya na makubaliano ya kimaslahi kabla ya kusaini kuichezea timu hiyo.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini kwa kuwa sio msemaji wa timu, mmoja wa viongozi wa nafasi za juu kwenye klabu hiyo alisema wamemuuza Sherman kwa dola 150,000 sawa na zaidi ya Sh milioni 300, ambapo klabu hiyo inatarajia kutuma fedha hizo wakati wowote baada ya kukamilika kwa taratibu za uhamisho wake.
“Ni kweli Sherman amefuzu vipimo vya afya na kusajiliwa kwa mkataba wa miaka mitatu na klabu ya Mpumalanga Black Aces, kila kitu kinakwenda vizuri na sasa tunamalizia taratibu za uhamisho wake ili wenzetu waweze kututumia malipo yetu tuweze kuyatumia kwa kuziba pengo la Sherman katika siku mbili zilizobaki kwenye usajili wetu,” alisema kiongozi huyo.
Kiongozi huyo alisema kuondoka kwa Sherman ni pengo kubwa kwa timu yao kwa sababu ndiyo kwanza alianza kuzoea Ligi ya Tanzania baada ya kuanza vibaya msimu wake wa kwanza lakini anaamini atafanikiwa huko anakokwenda na wao wapambana kuhakikisha wanamtafuta mtu sahihi wa kuziba nafasi yake.
“Alikuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Yanga lakini siku zote mpira haupo kwa ajili ya burudani na biashara, pia ndiyo maana tumemruhusu kuondoka na sisi tumepata pesa ambazo tutazitumia kuhakikisha tunaimarisha kikosi chetu katika sehemu ambazo tumeona zinamapungufu,” alisema kiongozi huyo.
Sherman alitua Yanga kwenye dirisha dogo la usajili msimu uliopita na kuonesha kiwango cha juu kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe, lakini baada ya hapo alionekana kushuka kiwango na kupoteza nafasi kwenye kikosi cha kwanza licha kumaliza msimu akifunga mabao sita kwenye ligi katika mechi 16 alizocheza mzunguko wa pili huku akijivunia ubingwa wa ligi ya Tanzania Bara msimu uliopita.
kuwa Musonye alikuwa akiipendelea timu hiyo licha ya kugoma kuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo, ambapo tayari timu hiyo ilishaonywa huko nyuma kwa kitendo kama hicho. Timu hiyo juzi iligoma tena kuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa mchezo wa fainali ya Kagame dhidi ya Azam FC, ambao walifungwa 2-0 na kushindwa kutwaa taji hilo.
Wakizungumza na waandishi kwa nyakati tofauti kuhusu ugomvi wao, viongozi wote wawili walikiri kushikana mashati, huku Musonye akisema lazima wawekeane heshima. Musonye hakusema sababu ya wao kushindwa kuelewana akijitetea kuwa katika masuala ya soka, kusuguana ni jambo la kawaida, hivyo walikuwa wakiwekeana heshima. “Tumeshayamaliza ilikuwa ni jambo dogo tunawekeana heshima. Kwenye soka mambo ndivyo yalivyo,”alisema.
Mgoi aliweka bayana kuwa Musonye alikuwa akitaka mgeni rasmi wa mashindano hayo awe Odinga ambaye alikuwa uwanjani hapo kushuhudia fainali za Gor Mahia na Azam. Alisema TFF haikuwa na taarifa kutoka serikalini kuwa Odinga atakuwa nchini kwa ajili hiyo, hivyo tayari walimuandaa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki kuwa mgeni rasmi.
Alisema baada ya TFF kuweka msimamo wao kama waandaaji wa mashindano kwa mgeni wao ambaye ni Sadiki, Musonye alianza kutoa maneno makali na kuanzisha vurugu. Hatahivyo, kama ilivyopangwa na TFF, Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam ndiye aliyetoa zawadi kwa Azam ambao ni mabingwa wapya wa Afrika Mashariki na Kati.
Pamoja na hilo, Mgoi alisema Musonye alikuwa akionesha upendeleo dhidi ya timu hiyo ya Kenya akiitetea timu ya Gor Mahia ambayo ilikiuka onyo ililopewa awali la kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwa imani za kishirikina.
Alisema timu hiyo ilivunja kitasa katika sehemu ambazo walikatazwa awali kuingia, na wao kutumia nguvu na kufanya lolote kwa vile tu walikuwa wakitetewa na katibu huyo wa Cecafa.
“Gor Mahia imekuwa na dosari nyingi ikiamini haiwezi kufanywa lolote na tunapomshirikisha Musonye hakutoa ushirikiano na badala yake amekuwa mtu wa kuitetea, ndio maana alipoonesha upendeleo wake, nasi tulisimama kuonesha uzalendo wetu,”alisema na kuongeza kuwa, timu hiyo imekuwa ikifanya uharibifu ikisaidiwa na kituo kilichokuwa kinarusha matangazo ya soka cha Supersport.
Kitendo hicho cha Gor Mahia kutoingia katika vyumba vya kubadilisha nguo sio cha kwanza, kwani katika mchezo dhidi ya Yanga walipita katika sehemu ambapo hupaki magari ya kurusha matangazo ya soka kwenye televisheni na kupewa onyo la kutorudia.

Kikwete azuia ‘ulaji’ trafiki

  RAIS Jakaya Kikwete ameliagiza Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, kuanzisha mara moja mfumo wa ulipaji faini kwa njia ya Benki na mitandao ya simu za mkononi ili kupunguza ushawishi wa vitendo vya rushwa kwa askari wa kikosi cha usalama barabarani nchini.
Pia, ameagiza kuanzishwa mfumo wa kuweka alama kwenye leseni za madereva wanaokiuka sheria na kutumia njia hiyo kuwafungia, ikiwa ni hatua mojawapo ya kudhibiti wimbi la ajali za barabarani hapa nchini.
Rais Kikwete alitoa agizo hilo jana katika viwanja vya Tangamano wakati alipokuwa akizindua Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani Kitaifa, inayofanyika mkoani Tanga, ikiwa imebeba kaulimbiu inayosema ‘Endesha Salama, Okoa Maisha’.
Alisema asilimia 56 ya ajali za barabarani, zinatokana na uzembe na ukosefu wa umakini kwa madereva na kwamba hatua hiyo inasababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali na hata kuathiri ustawi wa Kaya na Uchumi wa Taifa.
“Hivi mpaka sasa Baraza na Kikosi cha usalama barabarani wanashindwaje kutumia mifumo ya kidigitali kwa nini mpaka leo hakuna kamera barabarani? Kwanza ingesaidia kudhibiti ajali na uvunjaji wa sheria, lakini hata vitendo vya rushwa ambavyo navyo vinachangia ongezeko hili la wimbi wa ajali hapa nchini,” alisema Rais Kikwete.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2010 hadi 2014, jumla ya watu 19,264 walipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani na kwamba idadi ya ya waliokufa katika kipindi cha mwaka peke yake ni watu 3,534 sawa na idadi ya wanaopeteza maisha kutokana na ugonjwa wa malaria.
Kufuatia hatua hiyo, amelitaka baraza hilo kufanya mapendekezo ya marekebisho ya sheria za usalama barabarani hasa pale penye mapungufu ili kuweza kusaidia kudhibiti wimbi la ajali linalochangia upotevu wa nguvu kazi ya Taifa.
“Kikosi cha usalama barabarani kiongeze kasi ya kudhibiti ajali za barabarani na kuwachukulia hatua za kisheria Askari wanaojihusisha na vitendo vya rushwa….lakini lisilale katika kutoa elimu ya sheria za usalama barabarani hasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari,” alisisitiza Rais Kikwete.
Kwa upande Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani,Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, Mohamed Mpinga alisema lengo kuu la maadhimisho ya siku hiyo ni kuhamasisha matumizi salama ya barabara pamoja na kuwakumbusha watumiaji namna rahisi ya kutumia barabara ili kupunguza ajali zisizo za lazima.
“Tunapoadhimisha siku hii tunawakumbusha watumiaji kuwa ajenda kuu ya Taifa ni mapambano dhidi ya ajali za barabarani, jambo ambalo linaweza kuadhibitiwa kwa sababu ya uzembe na uvunjaji wa Sheria za Barabarani”,alisema Kamanda Mpinga.
Hata hivyo, alisema katika maadhimisho hayo Baraza limejipanga kufanya Mkutano Mkuu wa wadau utakaoshirikisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, sambamba na mafunzo kwa madereva 300 wa daladala na walimu 200 wa shule za msingi kwa lengo la kujenga uelewa kuhusu sheria za usalama barabarani.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Said Magalula alisema takwimu zinaonesha katika kipindi cha mwezi Januari mpaka Juni mwaka huu, ajali za barabarani zilikuwa 52 ambapo vifo vilikuwa 59 na majeruhi 68. Magalula alisema mkoa huo kwa mwaka 2014 ulifanikiwa kuingia katika tano bora kati ya mikoa ambayo imefanikiwa kudhibiti ajali za barabarani.

Nape: Wanaohama CCM ni sawa na mafuta machafu

    KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema wanachama waliokihama chama hicho wamejivua nguo mbele za watu na kwamba wapinzani wanaowachukua wanahangaika na mafuta machafu.
Aidha, amesema aliyekuwa Mbunge wa Segerea na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Milton Mahanga, alikuwa anatafuta sababu za kuihama CCM na anamtakia kila la heri, yeye na rafiki yake, Edward Lowassa.
Nape aliyasema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari katika Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba, Dar es Salaam, alipotakiwa kueleza kuhusu kuhama kwa Lowassa na Dk Mahanga ambao wote kwa nyakati tofauti wamekimbilia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Lowassa alijitoa CCM wiki moja iliyopita baada ya kukwama uteuzi wa CCM wa kuwa mgombea wake wa urais na kukimbilia Chadema ambako anatarajiwa kuwa mgombea wake wa urais na kuungwa mkono na Umoja wa Vyama vinne vya Upinzani (Ukawa).
Dk Mahanga naye alijitoa juzi baada ya kukwama katika kura za maoni jimboni Segerea. “Wanahangaika na oil chafu. Hawa ni wale wale kama ilivyokuwa Mrema (Augustino) mwaka 1995, akabebwa kiasi cha Mwalimu Nyerere kusema mwacheni abebwa.
Hebu jiulizeni wanaona ubaya wanapotoka, lakini mambo yakiwanyookea hawasemi, wakitoka ndio maneno mengi,” alisema Nape. Alisema kuondoka kwa Lowassa na wengine wachache, si jambo la kwanza kutokea CCM, na pia si la ajabu wala haliwezi kuwa la mwisho huku akimtuhumu Dk Mahanga kuwa alikuwa akitafuta sababu ya kuondoka CCM.
Akizungumzia mchakato wake Mtama, Nape alisema kulifanyika juhudi kubwa za mafisadi kuhakikisha anashindwa, lakini anashukuru ameshinda na kwamba endapo atapitishwa na chama hicho kugombea ubunge, ana hakika atashinda kwani ni mwadilifu na anayezingatia ya chama hicho ikiwamo kupiga vita rushwa.

Mbowe akiri Slaa ‘alimkataa’ Lowassa

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amekiri kuwa Katibu Mkuu wao, Dk Willibrod Slaa alitofautiana nao katika kumkubali aliyekuwa kada wa CCM, Edward Lowassa kujiunga nao, na sasa amepewa mapumziko.
Dk Slaa amekuwa ‘mafichoni’ tangu Lowassa akubaliwe Umoja wa vyama vinne vya upinzani (Ukawa) kujiunga nao na baadaye kujiunga na Chadema Julai 29, mwaka huu.
Inadaiwa kuwa Katibu Mkuu huyo wa Chadema anapinga kujiunga kwa Lowassa katika chama hicho bila masharti na tangu Waziri Mkuu huyo wa zamani ajiunge nao, ametoweka katika anga za siasa nchini na kumekuwa na maneno mengi kuhusu wapi alipo na kwa nini hajitokezi hadharani katika shughuli mbalimbali za chama hicho.
Lakini akifungua kikao cha Baraza Kuu la Chadema, Dar es Salaam jana ambalo moja ya kazi zake itakuwa kuchambua fomu za Lowassa ambaye ni mgombea pekee wa urais kupitia chama hicho cha upinzani, Mbowe alidai kuwa Dk Slaa ameomba kupumzika na amekubaliwa.
Alikiri kuwa Kamati Kuu ya chama, ilifanya vikao kadhaa kutafakari ujio wa Lowassa na kufanya mashauriano ya muda mrefu na kwamba halikuwa jambo jepesi. Alisema walifanya mashauriano yaliyoambatana na hadhi ya kitafiti ya kisayansi na kuridhika pasipo shaka kuwa ugeni wa Lowassa na wenzake Chadema ni sawa na mpango wa Mwenyezi Mungu uliopaswa kuungwa mkono ili uwasaidie katika azma yao ya kuwaunganisha wenzao wa Ukawa na Watanzania ili kufikia malengo ya pamoja.
“Katika hatua zote hizo tulikuwa sambamba na Mheshimiwa Dk Willibrod Slaa. Katika dakika za mwisho, Dk Slaa akatofautiana kidogo na Kamati Kuu. Tukajaribu kuzungumza naye kwa kina sana, hata jana nimekuwa na kikao na Dk Slaa kwa saa mbili, nimekuwa na kikao naye tena jana mchana,” alisema Mbowe.
Alisema kwa hali ilivyo kwa kuwa uchaguzi uko karibu, maji yakishafika wakati wa kupwa na kujaa, “hayamsubiri “Mbowe, hayamsubiri Slaa, hayamsubiri Baregu, maji yanasonga. Na Mgaya Kingoba

Magufuli leo mguu sawa kwa urais

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli leo anatarajiwa kuchukua fomu ya uteuzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kusaka wadhamini na kisha kuidhinishwa kuwa mgombea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Waziri huyo wa Ujenzi anatarajiwa kuchukua fomu saa sita kamili mchana, na kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye, mgombea huyo atafuatana na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan na viongozi waandamizi wa chama hicho tawala. Nape aliwaambia waandishi wa habari jana katika Ofisi Ndogo ya CCM, Mtaa wa Lumumba Dar es Salaam kuwa Dk Magufuli na msafara wake, wataondoka katika ofisi hizo saa tano asubuhi kwenda Ofisi za NEC zilizoko Mtaa wa Garden katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
“Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli atachukua fomu kesho (leo) saa sita mchana. Msafara wake utaondoka hapa (Ofisi Ndogo) saa tano kamili na ataambatana na mgombea mwenza na viongozi waandamizi akiwamo Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Katibu Mkuu, wajumbe wa Sekretarieti, Kamati za Siasa za Wilaya na Mkoa wa Dar es Salaam,” alieleza Nape.
Aliongeza kuwa msafara huo, utapitia katika barabara za Morogoro, Bibi Titi Mohammed na Ohio, na kurudi kwa njia hizo hadi Ofisi Ndogo Lumumba ambako Dk Magufuli atatoa neno la shukrani kwa wanachama, mashabiki na wapenzi wa chama hicho kikongwe na tawala nchini, na Watanzania kwa ujumla.
“Dk Magufuli akishachukua fomu atarejea hapa Ofisi Ndogo na kutoa neno la shukrani kwa kuzungumza na Watanzania wataokuwapo, wanachama na mashabiki wetu ifikapo saa saba mchana,” alieleza Nape ambaye mwishoni mwa wiki aliongoza katika kura za maoni za ubunge katika Jimbo la Mtama mkoani Lindi.
Dk Magufuli alishinda uteuzi wa kuwa Mgombea Urais wa CCM katika vikao vyake vilivyofanyika mjini Dodoma mapema mwezi uliopita, akiwashinda wenzake 38 ambao walikuwa miongoni mwa 42 waliochukua fomu.
Alikuwa miongoni mwa wagombea watano waliopitishwa na Kamati Kuu na kisha kupigiwa kura na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM akiwa na Dk Asha-Rose Migiro, Balozi Amina Salum Ali, January Makamba na Bernard Membe, ambapo yeye, Dk Migiro na Balozi Amina walishinda kwenda kupigiwa kura katika Mkutano Mkuu.
Katika Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika kwa siku mbili kuanzia Julai 11, mwaka huu, Dk Magufuli aliwashinda wanawake hao wawili na kupewa jukumu la kupeperusha bendera ya CCM Oktoba 25, dhidi ya vyama vingine.
Historia yake John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa tarehe 29 Oktoba 1959 wilayani Chato mkoani Kagera (sasa mkoa mpya wa Geita). Magufuli alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chato wilayani Chato mwaka 1967 na alihitimu mwaka 1974.
Alijiunga na Shule ya Seminari Katoke wilayani Biharamulo, ambako alisoma kidato cha kwanza na cha pili mwaka 1975 – 1977. Alihamishiwa Shule ya Sekondari Lake mkoani Mwanza, ambako alisoma kidato cha tatu na nne mwaka 1977 - 1978.
Masomo ya kidato cha tano na sita aliyapata mkoani Iringa katika Shule ya Sekondari Mkwawa kati ya mwaka 1979 na 1981. Alirudi Chuo cha Ualimu Mkwawa kusomea Stashahada ya Elimu ya Sayansi katika masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu.
Alisoma hapo mwaka 1981 – 1982. Baada ya kuhitimu hapo, alianza kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari Sengerema mkoani Geita, akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati kati ya mwaka 1982 na 1983.
Baadaye alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai - Desemba 1983), kisha kambi ya Makuyuni, Arusha (Januari hadi Machi 1984) na akamalizia kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi – Juni 1984).
Mwaka 1985 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati na alihitimu mwaka 1988. Mwaka 1989 - 1995 alifanya kazi katika kiwanda cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.) akiwa mkemia na wakati huohuo alianza masomo ya Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza, kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisoma kati ya mwaka 1991 na 1994.
Magufuli aliendelea na elimu ya juu zaidi kwa maana ya Shahada ya Uzamivu ya Kemia kuanzia mwaka 2000 hadi 2009, ambayo aliihitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa mhitimu wa shahada ya udaktari. Dk Magufuli ana mke na watoto kadhaa.
Dk Magufuli alichaguliwa kuwa mbunge wa Chato mwaka 1995, na aliposhinda Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Miundombinu. Katika uchaguzi wa mwaka 2000, Dk Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili.
Rais Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu . Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa mbunge kwa kipindi cha tatu na Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008, alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 alifanikiwa kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne na Rais Kikwete alimrudisha katika Wizara ya Ujenzi, ambako yupo hadi hivi sasa.

WAKRISTO WA ITALIA WAWEZESHA ZAHANATI YA KISASA VIKAWE




IMG_0282
Mkuu wa Masista Waabuduo Damu ya Kristo, Euprasia Julius akimtambulisha mgeni rasmi na meza kuu kwa wageni waalikwa na wanakijiji wa Vikawe (hawapo pichani) katika hafla ya ufunguzi wa Zahanati ya Da.Ma Africa Maria De Mathias (MDM) Vikawe, Kibaha.
MGANGA Mkuu wa halmashauri ya Mji Kibaha, Dk. Happniness Ndosi amepongeza shirika la masisita wa Waabuduo Damu ya Kristo kwa kufanikisha ujenzi wa zahanati ya kisasa katika kijiji cha Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Mganga huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa zahanati hiyo,pamoja na kuwapongeza amesema serikali itaendelea kushirikiana na mashirika yote kwa lengo la kuwezesha kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata kituo na kila wilaya kuwa na hospitali.
Aliwapongeza masista hao kwa kuonesha upendo na huruma kama Biblia inavyomsimulia msamaria mwema ambaye alikuta mtu aliyepigwa na majambazi na kumsaidia.
Aliahidi ushirikiano wa serikali katika kufanikisha usajili wa zahanati hiyo na kuendelea kuisaidia hatua kwa hatua hadi inakuwa kituo mpaka watakapofanikisha safari yao ya kuwa hospitali kubwa ya kisasa.
Mganga huyo pamoja na kutoa ahadi hiyo aliwataka wananchi wa Vikawe kutumia huduma hiyo na kwamba zahanati hiyo itakapohitaji msaada wa gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) wataletewa kuchukua mgonjwa na kumfikisha panapohusika.
Zahanati hiyo ya DA.MA Africa imejengwa kwa ufadhili wa wakristo wa Italia chini ya usimamizi wa Muitalia, Germano Frioni.
Akitoa salamu zake Muitalia huyo amesema kwamba anawashukuru wakazi wa Vikawe kwa kumpa nguvu ya kusonga mbele hasa kwa kutambua kwamba yeye na marafiki zake wamefanyakazi usiku na mchana kutafuta fedha kwa ajili ya kusaidia marafiki wa Afrika.
Alisema atajitahidi kufanya kila linalowezekana kuhakikisha changamoto za zahanati hiyo zinafanyiwa kazi.(VICTOR)

Aliwaomba wananchi wa Tanzania kuendelea kumuombea yeye na wenzake kama Papa Francis anavyoagiza ili malengo ya safari ya kuwapo duniani yafanikiwe.
Alisema kwamba watoto wake Daniel na Marco (kwa sasa wote ni marehemu) ambao ndio kifupi cha zahanati hiyo DA.MA wamemfanya kujitambua na kusaidia wengine katika kuonesha upendo.
Aidha alisema kwamba ataendelea kukumbuka Vikawe kwani alifika mara ya kwanza mwaka 2005 na kuona hali ilivyokuwa ambapo sasa lipo jengo la zahanati hiyo likiwa limekamilika.
Wazo la ujenzi wa zahanati hiyo , lilitolewa na wananchi wa Vikawe kwa Masisita Waabuduo Damu ya Kristo mwaka 2004 wakati wakiwa katika eneo hilo baada ya kununua ekari 40 kwa ajili ya kilimo mwaka 1994.
Alisema pamoja na maombi hayo na wao wenyewe kutambua kwamba kuna mahitaji makubwa ya huduma ya afya japokuwa kuna zahanati ya serikali, hawakuweza kutekeleza maombi ya wanavijiji hadi mwaka 2011 walipofanikiwa kupata ufadhili kutoka Italia na kuanza ujenzi mwaka 2013.
Katika risala yao walisema kwa ushirikiano kati yao na wafadhili hao wamefanikiwa kuwapo kwa zahanati hiyo yenye mahitaji yote ya msingi kwa mujibu wa taratibu za serikali na kuzidi.
Msoma risala alisema kwamba wataendelea kupanua miundombinu mpaka zahanati hiyo ifikie ngazi ya cha afya na baadae hospitali.
Pamoja na ujenzi wa zahanati hiyo ya kisasa masisita hao wameanzisha shule ya awali kuwaandaa wanafunzi wa darasa la kwanza.
Wamesema kwamba wanaamini kwamba wataendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa afya katika kuimarisha huduma za hospitali hiyo.
Zahanati hiyo pamoja na vifaa tiba pia ina raslimali ya visima vya maji ya mvua ujazo zenye ujazo wa lita laki moja na kingine lita 49 elfu, wanatumia umeme wa sola na jenereta .
Walisema kwamba wanachangamoto ya kukosa umeme wa Tanesco, barabara nzuri na nyumba za wafanyakazi.

Kyela ni Mwakyembe tena

WAZIRI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela anayemaliza muda muda wake, ameshinda kura za maoni katika jimbo hilo akiwabwaga wagombea wenzake tisa waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Katibu wa CCM Wilaya ya Kyela, Eva Degeleki alisema Dk Mwakyembe aliibuka mshindi kwa kujizolea kura 15,516 akifuatiwa na George Mwakalinga aliyeambulia kura 4,905.
Degeleki alisema aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Gabriel Kipija alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 2,301 na wagombea wengine waliofuata na kura zao kwenye mabano walikuwa ni Asajile Mwambambale (994), Vincent Mwamakimbula (881), John Mwaipopo (785), Ackim Mwakipiso (601), Benjamin Mwakasyege (442), Dk Leonard Mwaikambo (283) na Gwakisa Mwandembwa (263).

Mbowe: Nitamzungumzia Dk Slaa muda ukifika

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amezungumzia kukosekana kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa katika vikao vya chama hicho vinavyoendelea jijini, akisema: “Nitazungumzia suala hilo muda muafaka ukifika.”
Mbowe alisema hayo jana katika Hoteli ya Ledger Plaza Bahari Beach kilipokuwa kinafanyika kikao cha Kamati Kuu ya Chadema jana.
“Siwezi kusema zaidi ya hapo,” alisema Mbowe alipoulizwa sababu za kutokuwapo Dk Slaa katika vikao hivyo muhimu na kuongeza atatoa baadaye, mrejesho wa kikao hicho.
Kauli hiyo ya Mbowe haikuondoa wingu zito lililotanda Chadema baada ya kutoonekana hadharani kwa kiongozi huyo katika matukio manne muhimu ya chama hicho kikuu cha upinzani, tangu waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ajiunge nacho.
Tofauti na Dk Slaa, Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika alionekana jana kwa mara ya kwanza katika kikao hicho na kufuta uvumi uliokuwa umesambaa kuwa alikuwa na mpango wa kuachana na Chadema kama inavyodaiwa kwa Dk Slaa.
Viongozi hao walianza kutoonekana katika shughuli za chama tangu Lowassa alipojiunga na Chadema Julai 28 na kukabidhiwa fomu ya kugombea urais Julai 30 na juzi Agosti Mosi alipozirejesha.
Hata hivyo, viongozi waandamizi wa Chadema wamesema suala la kutokuwapo kwa Dk Slaa halipaswi kukuzwa kwa kuwa ‘anafanya kazi nyingine za chama.’
Alipoulizwa jana, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema: “Suala la kutokuwapo Dk Slaa ni kitu cha kawaida, anafanya kazi nyingine huko, lakini pia kuna wasaidizi wake hapa ambao ni sisi manaibu. Mlikuwa mnazungumzia Mnyika naye haonekani, si huyo. Hatuwezi kuendelea kujibu ‘rumors’ (uzushi) wa kwenye mitandao… nyie subirini si tupo mtaona kama yupo au la.”
Mnyika atinga kikaoni
Jana, Mnyika alionekana katika viwanja vya hoteli hiyo lakini alikataa kuzungumzia kwa undani suala hizo.
“Siwezi kuzungumza chochote,” alisema Mnyika na hata alipoulizwa ni lini atawaeleza Watanzania juu ya kutoonekana kwake alisisitiza mara tatu kuwa “Siwezi kuzungumza chochote.”
Chama hicho kinaendelea na mfululizo wa vikao vya vyombo vya juu ambapo leo kinatarajia kutafanya kikao cha Baraza Kuu kabla ya Mkutano Mkuu kesho kumpitisha mgombea wa urais kesho.
Kura za maoni Kibamba zaahirishwa
Mchakato wa kura za maoni wa kumpata mgombea wa ubunge wa chama hicho katika Jimbo Kibamba utafanyika leo baada ya kuahirishwa juzi.
Kaimu Katibu wa Chadema Mkoa wa kichama Kinondoni, Rose Mushi alisema kura hizo zitapigwa leo kuanzia saa nne asubuhi, Kimara Baruti. “Kila kitu kinakwenda vizuri, nadhani kesho (leo), tutafanya mchakato huu wa kura za maoni, kama kutakuwa mabadiliko nitakutaarifu,” alisema Mushi.
Awali, Mratibu wa Chadema Kanda Pwani, Casmir Mabina alisema: “Jana (juzi), tulishindwa kufanya kwa sababu mmoja wa watia nia alikuwa mgonjwa. Hakupata taarifa za mchakato huo, tukatumia demokrasia ya kuahirisha.”
Mwenyekiti wa Jimbo la Ubungo, Boniface Jacob alisema kura za maoni katika jimbo hilo (Kibamba) huenda zikafanyika leo baada ya kupokea taarifa kutoka kanda. “Sisi kazi yetu ni kuratibu mchakato wa kura za maoni ila maelekezo yote yanatoka juu, inawezekana ikiwa kesho (leo) jioni sina uhakika,“ alisema Jacob.
Juzi, hali ya sintofahamu iliwakumbuka wajumbe na watia nia wa jimbo hilo baada ya kufika kwenye ukumbi wa mikutano na kuambiwa kuwa mchakato wa kura za maoni umeahirishwa kwa madai kuwa mmoja ya watia nia hakupewa taarifa.
Hatua hiyo ilizua minong’ono miongoni wa wajumbe na watia nia ambao waliokuwa wamejiandaa kwa mchakato huo wakidai kuna hujuma zinataka kufanyika.
(CHANZO: MWANANCHI)

20 CCM washikiliwa kwa tuhuma za rushwa

                                TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Nkasi mkoani Rukwa, inawashikilia wanachama 20 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwemo diwani wa Viti Maalumu (CCM) aliyemaliza muda wake, wakituhumiwa kutoa na kupokea rushwa.
Diwani huyo, Matrida Londezya ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) wilaya ya Nkasi, anatuhumiwa kuwashawishi wana CCM 20 kwa kuwapatia kiasi cha Sh 2,000 kila mmoja ili achaguliwe kuwa diwani wa kata ya Nkomolo kwa tiketi ya CCM kwenye kura za maoni zinazofanyika leo.
Kamanda wa Takukuru wilaya ya Nkasi, Samson Bishati alithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao juzi saa 3:00 usiku wakiwa katika nyumba ya mtu aliyetajwa kuwa Victor Sadala iliyopo katika eneo la kata ya Nkomolo mjini Namanyere.
Sadala, ambaye anadaiwa kuwa wakala wa mgombea ni miongoni mwa watuhumiwa 20 wanaoshikiliwa na taasisi hiyo ya kuzuia rushwa nchini.
“Nilikuwa na maofisa wenzangu watatu katika doria ya kuwatambua, kuwabaini na kuwakamata wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa katika mchakato wa kura za maoni za madiwani na wabunge wilayani Nkasi,” alisema na kuongeza kuwa mtoa siri wao aliwataarifu kuwa kuna wanachama wa CCM wapatao 20 wamekusanyika kwenye nyumba ya Sadala aliyewaita ili kuwashawishi wampendekeze Londezya achaguliwe katika kura ya maoni.
Alisema kwa mujibu wa taarifa walizozipata ni kuwa mkusanyiko huo ulilenga kugawana fedha zilizotolewa na mgombea huyo wa udiwani ili wampatie upendeleo maalumu kwenye kura za maoni na baada ya kupokea taarifa hiyo walikwenda moja kwa moja eneo la tukio na kukuta watu hao na mgombea ambapo waliwakamata na wanawashikilia.
Kwa mujibu wa Bishati, walipofika eneo la tukio watuhumiwa waliwekwa chini ya ulinzi ambapo mwenye nyumba alijaribu kukimbia kwa hofu, lakini ilishindikana na sasa watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.

Utumiaji dawa za kulevya waongezeka

MATUMIZI ya dawa za kulevya nchini yameongezeka kwenye mikoa 12 nchini yakionesha dawa aina ya heroini na bangi zikiongoza kwa kutumiwa zaidi.
Utafiti uliofanywa kwenye mikoa 12 nchini iliyopo pembezoni mwa barabara kuu zinazounganisha miji au nchi nyingine, zikiwa kwenye hatari zaidi ya wananchi wake kutumia dawa hizo.
Mikoa hiyo ni Mtwara, Dodoma, Morogoro, Pwani, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya, Shinyanga, Geita na Kigoma. Wakiwasilisha matokeo ya utafiti huo juzi Dar es Salaam, watafiti waliohusika kwenye kazi hiyo, walisema kazi hiyo ilifanywa kati ya Julai 2013 na Agosti 2014 katika mikoa hiyo.
Mmoja wa watafiti hao, Moza Makumbuli alisema kutoka mikoa hiyo 12, watumiaji wa dawa hizo wanapata shida kubaini aina ya dawa kati ya heroini au kokeni, bali huita dawa hizo unga.
Katika mkoa wa Tanga, utafiti umebaini matumizi ya dawa za kulevya yamesambaa kwenye miji midogo na vijijini nje ya mji kwenye maeneo ya kandokando ya barabara ya Segera,Tanga.
Mkoani Mtwara, utafiti ulionesha watumiaji wa dawa kwa njia ya kujidunga ni wachache ukilinganisha na wavutaji wa dawa hizo kwenye Manispaa ya mkoa huo, lakini pia utafiti umeonesha Mji wa Masasi una watumiaji wa dawa hizo.

Takukuru yamsafisha Nape

Kamanda wa Takukuru mkoani, StevenChami
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani hapa, imekanusha tuhuma za rushwa zilizoelezwa na baadhi ya vyombo vya habari dhidi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM), Nape Nnauye.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi yake, Kamanda wa Takukuru mkoani hapa, Steven Chami alisema, taasisi hiyo haikumkamata Nape kwa sababu ya kuhusika na rushwa, bali ilitaka kujiridhisha na kiwango cha fedha kilichokuwa kikitolewa kwa mawakala.
Alisema, “Uhakiki ulifanywa kwa watu wote walioomba ridhaa ya kugombea nafasi mbalimbali mkoani humu, ikiwa ni pamoja na ubunge, ambao Nnauye na wengine waliomba."
Kutokana na maelezo yake, Nape alikuwa miongoni mwa wanasiasa walioomba ridhaa ya CCM kugombea ubunge katika jimbo la Mtama, na alikuwa pia miongoni mwa watangaza nia walioingia kuchukua fedha katika Benki ya NMB ya mjini hapa, iliyotajwa na vyombo vya habari.
Alifafanua kuwa, kitendo cha maofisa wa Takukuru kumfuata Nnauye ili wajiridhishe na kiwango cha fedha alichokitoa kwa ajili ya mawakala, kilichukuliwa kuwa ni kumkamata kwa rushwa jambo ambalo si kweli.
“Vijana wangu walimuomba Nnauye aongozane nao hadi ofisini ili wahakiki kiasi cha fedha alichokuwa amekitoa benki. Alifanya hivyo na kutumia dakika kati ya 30 na 45 kutoa maelezo yaliyowaridhisha maofisa wa Takukuru waliomwachia baada ya mahojiano mafupi. “...Ninapenda kuwathibitishia kuwa, Nnauye alikuwa na kiwango cha kawaida cha fedha ambacho kinaruhusiwa kutolewa kwa mawakala. Haikuwa rushwa kama ilivyopotoshwa na baadhi ya wanahabari walioandika na kutangaza habari hiyo,” Chami alisema na kuongeza kuwa alikutwa na Sh milioni tatu tu.
Alisema, Nnauye aliieleza Takukuru kuwa fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya kuwalipa mawakala wake 156, aliowaandaa kusimamia uchaguzi katika vituo vyote jimboni humo.
Kutokana na kadhia hiyo, Chami alivionya vyombo vya habari kuwa makini kuepuka kupotosha jamii kwa sababu, kufanya hivyo kunaweza kukaribisha uvunjifu wa amani.

NEC yaandikisha watu milioni 21

Jaji mstaafu Damian Lubuva
   TUME ya Uchaguzi (NEC), imesema imeandikisha zaidi ya watu milioni 21 nchini tangu uandikishaji uanze Februari 23, mwaka huu na kwamba, Dar es Salaam pekee, wameandikishwa watu zaidi ya milioni mbili.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema juzi Dar es Salaam kuwa, uandikishaji wa wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR) unaendelea jijini humo hadi Agosti 8.
Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, baada ya siku hizo zilizoongezwa, hakutakuwa na muda mwingine utakaoongezwa.
“Tumieni muda ulioongezwa kujiandikisha, vinginevyo mtaikosa haki yenu ya kupiga kura kwa sababu ya kutoandikishwa katika Daftari la Wapigakura,” Jaji Lubuva alisema.
©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved