WAKATI baadhi ya wabunge wakisema hatua ya serikali kutaka kuongeza
kodi kwenye mafuta itapanda gharama za maisha na kuongeza ugumu wa
maisha kwa Watanzania, Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP)
ameimwagia sifa bajeti na kusema wakati umefika wa kuondokana na
serikali ya vibatari na koroboi.
Akichangia mjadala wa bajeti ya mwaka 2015/16, Cheyo alisema
amefurahishwa na bajeti kutokana na azima ya kupeleka umeme vijijini,
kujitegemea na kuachana na utegemezi.
“Serikali inayotaka maendeleo ya koroboi na kibatari ni kurudi nyuma,
kwanza mafuta ya taa yana ‘kabonmonoksaidi’ ambayo ni sumu, mimi
ningekataza matumizi ya mafuta ya taa majumbani na badala yake wangekuwa
wana ‘kanda’ (kubonyeza swichi za kuwasha umeme.”
Alisema Serikali ijayo, iwe serikali ya gesi na umeme wa jua ili
kuachana na matumizi ya mkaa, na mafuta ya taa vijijini, hivyo ongezeko
la kodi katika mafuta ya taa ni jambo sahihi na kusifia hatua ya
serikali ya kuwekea uzio fedha za miradi.
“Tukijitegemea angalau tutaachana na upuuzi wa kuomba serikali za
ughaibuni, na misaada yenyewe inakuja na masharti, ukikosea katikati
wanakata hela. Aliongeza: “Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Bajeti walipokuja
wafadhili niliwaambia wazi kama kweli ni marafiki watuache tufanye yale
tuliyokubaliana hata tukikosea katikati ya bajeti basi wapunguze bajeti
ijayo. “Ni lazima tutafute njia ya kujitegemea, ni mwenendo unaofanya
nchi kuwa huru. Kutegemea misaada kuna siku tutaletewa masharti ya ndoa
za jinsia moja, nikiwa mzima tusifike huko.”
Alisema yeye ametumia fedha za jimbo kwa kuweka umeme wa jua katika
shule za sekondari 21 katika wilaya ya Ikilima, jambo ambalo litasaidia
kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Juzi jioni wakichangia mjadala wa bajeti, baadhi ya wabunge walisema
asilimia 80 ya Watanzania wanaoishi vijijini wanategemea mafuta ya taa
kwa ajili ya kuwasha taa nyakati za usiku, huku mafuta ya petroli na
dizeli yatachangia kupaa kwa bidhaa na mfumuko wa bei.
No comments:
Post a Comment