MBUNGE wa Kinondoni, Iddi Azzan (CCM) ameitaka Serikali kuhakikisha
inatenga bajeti ya michezo kama nchi inataka kupata mafanikio katika
nyanja hiyo.
Aidha, ameutaka uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
kutekeleza wajibu wao ipasavyo kama ilivyokuwa kwa uongozi uliopita ili
kupata mafanikio katika mchezo huo na kuondoa malalamiko yaliyopo sasa.
Akichangia Bajeti ya Serikali ya mwaka 2015/16, Azzan alisema hali ya
sasa ya serikali kutopanga bajeti yoyote kwa ajili ya michezo,
hakutaiwezesha Tanzania kupata ushindi katika nyanja ya michezo.
Alisema miaka ya nyuma, Tanzania ilikuwa ikifanya vizuri katika
michezo mbalimbali ikiwamo soka na riadha, lakini sasa imekuwa haifanya
vizuri kutokana na kutotengewa fedha za kutosha.
“Tanzania sasa inatia aibu katika michezo, mpira wa miguu ni aibu
tupu na michezo mingine pia haifanyi vizuri. Tukiimarisha nyanja hii
itakuwa na faida kama ilivyokuwa siku ya nyuma na kuwa chanzo cha
mapato,” alisema Azzan aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa
wa Dar es Salaam (DRFA) na cha Kinondoni (KIFA).
Aidha, Azzan ameutaka uongozi wa TFF kutakiwa kubadilika katika
utendaji wa kazi kwa kuwa imekuwa ikilalamikiwa na wananchi na wamekuwa
wakifanya mambo mengi yasiyofaa.
“TFF wanalalamikiwa sana na wananchi kuna haja ya kubadilika,
wanatakiwa kuwajibika na kupata mafanikio kama uongozi uliopita,”
alisema Azzan aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa timu ya Tanzania Stars.
Kwa sasa TFF iko chini ya uongozi wa Rais wa shirikisho hilo, Jamal
Malizi ambaye alishika kijiti hicho kutoka kwa uongozi wa Leodegar Tenga
aliyeongoza kwa mihula miwili.
Kuhusu kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij, Azzan alisema matatizo ya
kocha ni kero na kuwa uwezo wake ni mdogo. Alisema tangu kuanza
kufundisha Taifa Stars, ushindi kwa timu hiyo ni asilimia 10 na imefanya
vibaya kwa asilimia kubwa.
Katika kampeni ya kutafuta kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika (AFCON), Taifa Stars ilifungwa mabao 3-0 na Misri mwishoni mwa
wiki na Tanzania inaburuza mkia katika kundi G lenye pia Nigeria na
Chad.
No comments:
Post a Comment