SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema Zanzibar haiwezi kuwa
mwanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa sababu
imepoteza mamlaka kamili ya dola kwa kuungana na Tanganyika na kuzaliwa
kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Aprili 26, 1964.
Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk
alisema hayo wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Wawi, Saleh
Nassor Juma (CUF) aliyetaka kufahamu suala la uanachama wa Zanzibar
katika Fifa na mikakati ya kuendeleza soka la ufukweni.
Akifafanua zaidi, Mbarouk alisema uwakilishi wa Zanzibar katika
mashirika ya kimataifa unafanywa chini ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa mujibu wa makubaliano ya muundo wake na mkataba wa Muungano
wa mwaka 1964.
Alisema katika masuala ya soka ya kimataifa, Zanzibar inawakilishwa
na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kutumia tiketi ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa muundo wa Muungano uliopo sasa.
Alisema mashirikiano ya Zanzibar kupitia Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) pamoja na TFF ni makubwa katika Fifa.
“Huo ndiyo ukweli wenyewe.... Zanzibar haiwezi kuwa mwanachama wa
Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) kwa sababu sio nchi kamili
inayojitegemea kwa mujibu wa makubaliano yetu tunashirikishwa katika
masuala hayo na TFF,” alisema Waziri huyo anayesimamia sekta ya michezo.
Alisema wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walikuwa na nafasi nzuri
ambayo walipaswa kuitumia wakati walipokuwa katika Bunge Maalumu la
Katiba kama wanataka mabadiliko makubwa katika suala la Muungano na
muundo wake.
“Mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba ilikuwa moja ya fursa nzuri ya
Wazanzibari kutaka mabadiliko makubwa ya muundo wa Muungano ikiwemo
suala la soka na Fifa, lakini wajumbe hawakuitumia fursa hiyo,” alisema.
Hata hivyo, Mbarouk alisema Zanzibar sasa imeanza kushiriki katika
mchezo wa soka la ufukweni na kupata mafanikio makubwa kwa kushirikiana
na TFF katika kutoa wachezaji mbalimbali wanaoshiriki katika michezo
hiyo.
Alisema kwa Zanzibar zipo timu 12 zinazoshiriki katika ligi ya soka la ufukweni kwa upande wa Unguja na Pemba.
No comments:
Post a Comment