Kamara afuzu Yanga..

MCHEZAJI mpya anayefanya majaribio kwa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, Lansana Kamara amefuzu majaribio hayo baada ya uongozi wa Yanga kuridhishwa na kiwango chake.
Ni wiki moja imepita tangu mchezaji huyo ajiunge kwenye mazoezi ya Yanga akifanya majaribio na kikosi hicho kusaka nafasi ya kusajiliwa msimu ujao.
Akizungumza na kituo kimoja cha redio jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha alisema Kamara ni aina ya mchezaji ambaye Yanga inamhitaji kwani ana kiwango kizuri kitakachowasaidia kufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali ya kimataifa.
“Kamara ni mchezaji mzuri na hata Kocha ametueleza kuwa anafaa kwani ana kiwango kizuri, tunamhitaji na ikiwa mambo yatakuja vizuri hasa katika kuongezwa idadi ya wachezaji wa kigeni tutamsajili,” alisema Dk Tiboroha akimzungumzia mchezaji huyo raia wa Sierra Leone.
Dk Tiboroha alisema kwa sasa wanasubiri tamko la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama wataongeza idadi ya usajili wa wachezaji wa kigeni ndipo wachukue hatua mara moja.
Alisema iwapo idadi itaongezwa watamsajili mchezaji huyo, lakini ikiwa hawataongeza, tayari wana wachezaji watano wa kigeni wenye mikataba labda itokee apunguzwe mmoja na nafasi ichukuliwe na kiungo huyo aliyeonesha uwezo.
Yanga inao Amissi Tambwe (Burundi), Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite (Rwanda), Andrey Countinho (Brazil) na Kpah Sherman (Liberia) katika orodha ya wachezaji wake watano wageni.
Hivi karibuni, TFF ilitoa waraka kwa klabu kupendekeza idadi ya wachezaji kisha Kamati ya Utendaji ikae na kulijadili, agizo ambalo klabu mbalimbali zilipokea kwa mikono miwili na kuonesha utayari wa ongezeko.
Yanga tayari walipendekeza idadi ya wachezaji wanane, wakati klabu nyingine kama Azam FC ilisema idadi yoyote itakayoongezwa watafurahia ili wasajili wachezaji wenye uwezo watakaowasaidia katika michuano ya kimataifa.
Kuhusu maombi ya klabu hizo, Katibu Mkuu wa TFF Selestine Mwesiga aliliambia gazeti hili jana kuwa Kamati ya Utendaji inatarajiwa kukutana Jumamosi ya wiki hii Zanzibar kwa ajili ya kupitia mapendekezo yote.
Alisema baada ya kikao hicho watatoa tamko lao kama maombi hayo yatapitishwa ama yatakuwa yamekataliwa kwa kuwa dirisha la usajili limeshafunguliwa na timu zinasubiri tamko hilo kuchukua hatua.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved