RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameishukuru Serikali ya China
kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya
ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwaleta madaktari kila baada ya miaka
miwili hapa nchini.
Dk Shein aliyasema hayo jana Ikulu mjini Zanzibar katika mazungumzo
kati yake na madaktari 25 kutoka China waliomaliza muda wao wa kazi
nchini waliofika Ikulu kwa ajili ya kumuaga Rais wakiongozwa na Balozi
Mdogo wa nchi hiyo anayefanya kazi zake Zanzibar, Xie Yunliang.
Katika mazungumzo hayo, Dk Shein alisema utamaduni wa kuleta
madaktari kutoka China ni wa kihistoria ulioanzia mwaka 1965 na
umeendelea kuwepo.
Dk Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wake
wanathamini na wanazipenda huduma mbalimbali zinazotolewa na madaktari
hao.
Pamoja na hayo, Dk Shein alitoa pongezi zake kwa Serikali ya China
chini ya Rais Xie Jingping kwa kuendelea kuisaidia Zanzibar katika
miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa Hospitali ya Abdalla
Mzee Mkoani Pemba, Ujenzi wa Uwanja wa Mao tse Tung na ujenzi wa jengo
jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amaan Karume Zanzibar.
Kiongozi wa madaktari hao 25, Dk Liu Yaping akitoa shukurani kwa
niaba ya madaktari hao alisema wamefurahia mazingira ya kufanyia kazi
nchini na ushirikiano walioupata kutoka kwa madaktari wazalendo wa
Zanzibari kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment