BAADA ya aliyewahi kuwa waziri katika wizara mbalimbali awamu ya
kwanza, George Kahama kutangaza hadharani kumuunga mkono Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuteuliwa na chama
chake kugombea Urais, naye Waziri Mkuu wa zamani, David Msuya
amejitokeza hadharani kumuunga mkono Waziri Membe.
Msuya akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake kijijini
Mwanga, Same jana, alisema amejiridhisha na uongozi wa Membe huku
akieleza kuwa hakuna sababu ya CCM kushindwa kumteua kuwa mgombea wake.
“Mwanzoni mjadala huu wa wagombea ulipoanza watu walikuwa wakijadili
majina ya watu, lakini mimi nikasema hapana, tujadili sifa na si majina
na bahati nzuri chama kupitia kwa Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa
chama tayari ameziweka hadharani nadhani ni kumi na tatu.
“Huwezi kutangaza nia ama kutaka kuongoza kupitia CCM kama hujajipima
na sifa hizo lakini mimi kwa sifa hizi kumi na tatu za chama sioni
sababu hata moja ya chama kushindwa kukuteua maana ninaona unazo zote,”
alisema Msuya na kuongeza; “Mimi nakuunga mkono kwa nguvu zote maana
umefaulu kinachotakiwa sasa ni wewe kufuata taratibu za chama kisha
usubiri maamuzi ya chama mwezi ujao lakini sisi hapa Mwanga tunakupa
baraka zote na ufanikiwe safari hii ambayo kwa kweli mimi ninaamini
hakuna Mtanzania atakayejuta wewe ukiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.”
Msuya kama alivyo Sir Kahama anatajwa kuwa miongoni mwa wazee pekee
waliosalia nchi hii wenye heshima kubwa kutokana na kustaafu nyadhifa
zao wakiwa hawana kashfa za ukosefu wa maadili katika utumishi wa umma.
Akizungumzia suala la maadili Msuya alisema; “ kusema kweli suala la
uadilifu linawakera sana Watanzania hasa hili eneo la rushwa kubwa na
ufisadi ndio maana anapojitokeza mtu asiye na sifa hiyo ya rushwa na
ufisadi ni rahisi sana kumkubali, tunakupa baraka zote ili uendeleze
pale walipofikia wenzio ukianza na waasisi.”
Naye Membe akijibu maoni hayo ya Msuya alisema; “ ninashukuru sana
mzee wetu, ninashukuru kwa kunitia moyo katika safari hii iliyoanza kama
ndoto yangu na sasa ni ndoto yako pia na ninaamini ni ndoto ya
Watanzania sasa kupata kiongozi anayeweza kuendeleza mazuri yaliyofikiwa
na uongozi uliotangulia na sasa tunataka tuwe na uchumi wa viwanda
unaobebwa na kilimo.”
Membe alipita kumjulia hali Mzee Msuya huku akiwa katika ziara ya
kutafuta udhamini wa wanachama ili kutimiza moja ya masharti na kanuni
za chama hicho.
No comments:
Post a Comment