JK aeleza atakayofanya akitoka Ikulu

RAIS Jakaya Kikwete, amesema mara baada ya kung’atuka madarakani baadaye mwaka huu, ataanzisha taasisi yake itakayojikita zaidi katika kushughulikia masuala yanayowagusa watoto, wanawake na maendeleo ya kilimo.
Aidha, amesema angependa kutumia muda wake mwingi kufanya kazi ya kuwasaidia Watanzania kuinuka kiuchumi, badala ya majukumu mengine ya kimataifa, yakiwemo ya usuluhisho wa migogoro.
Aliyasema hayo hivi karibuni mjini The Hague, Uholanzi katika mkutano wake na Watanzania waishio nchini humo uliokuwa na lengo la kuzungumza nao na pia kutumia fursa hiyo kuwaaga rasmi kwa kuwa muda wake wa kuwa madarakani utaofikia ukomo kwa mujibu wa Katiba Oktoba mwaka huu.
Akiwa katika Hoteli ya Crownie Plaza, alisema anakusudia kuanzisha taasisi itakayosaidia makundi mbalimbali, hasa watoto na wanawake na pia kundi la wakulima ambao kutokana na wingi wa karibu asilimia 80 ya Watanzania wote, wakiinuliwa watakuwa na nafasi kubwa ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Rais Kikwete aliyekuwa katika siku ya pili ya ziara yake Uholanzi, baada ya kuwa amefanya hivyo Finland na Sweden, alilazimika kuyasema hayo muda mfupi baada ya umoja wa Watanzania hao kumzawadia begi la kubeba makabrasha, huku wakisema wanaamini baada ya muda wake wa uongozi kwisha, atakabidhiwa majukumu mengi ya kimataifa kutokana na heshima kubwa aliyojijengea duniani.
Walitolea mfano kukabidhiwa jukumu la kusuluhisha migogoro ya kisiasa, ikiwemo ya Kenya, kuwa ni uthibitisho wa kuaminiwa kwake na jumuiya ya kimataifa.
Alikabidhiwa pia ngao maalumu ya ushupavu katika uongozi, na kitenge kwa ajili ya mke wa Rais, Mama Salma, lakini akizungumzia zawadi hizo, alishukuru na kusema hilo la jukumu la kusuluhisha migogoro ya kimataifa si kipaumbele chake, kwani anafikiria zaidi kuwatumikia Watanzania kwa mrengo mwingine.
Aidha, alisema mara kadhaa amekuwa akipenda kuwatumikia Watanzania, ndiyo maana kabla ya kuwa Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, aliwahi kupewa heshima ya kufanya kazi ya kimataifa huko Algiers, Algeria lakini alikataa.
“Niwe muwazi, hayo ya kimataifa nisingependa kuyafikiria sana, lakini baada ya kustaafu nafikiria kuanzisha Foundation (Mfuko) utakaojikita kukabiliana na madhila yanayowakuta watoto, wanawake na wakulima…hiyo ndiyo kiu yangu kwa sababu makundi haya yanahitaji msaada kweli kweli…,” alisema.
Kiu ya Rais Kikwete ya kujikita katika kilimo ilionekana dhahiri katika vikao mbalimbali vya kazi katika ziara yake, kwani alihimiza nchi wahisani kuiamini Tanzania na kuimiminia misaada, hasa yenye lengo la kuinua kilimo kwa kuwa misaada yao siku zote inatumika vizuri.
Waziri Koenders aliahidi Serikali ya Uholanzi kuendelea kuisaidia Tanzania, huku akisisitiza italifanyia kazi ombi la Rais Kikwete katika kukuza Kilimo nchini Tanzania.
Hata alipokutana na Mfalme Willem-Alexander na pia Waziri Mkuu, Mark Rute, Rais Kikwete aliendelea kutoa shukrani kwa misaada ya maendeleo na kuitaka Uholanzi kuendelea kuisaidia Tanzania.
Katika sekta ya kilimo, Uholanzi moja ya nchi ndogo kijiografia, lakini zilizopiga hatua kubwa kiuchumi, inatamba katika kilimo ikiwa ya pili kwa uzalishaji wa mazao ya chakula duniani, aidha ndiyo inayotoa theluthi moja ya bidhaa za mboga katika nchi za Jumuiya ya Ulaya.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved