Katiba isiwe kigezo cha kugawa wananchi -Nape

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amehimiza mshikamano nchini akihadharisha Katiba isiwe kigezo cha kugawa wananchi na kusahaulisha kushughulikia matatizo yanayowakabili.
Nape alitoa rai hiyo juzi wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Ngara, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana mkoani Kagera. “Tuna sababu gani ya kugombana, tuna sababu gani ya kutofautiana?
…tunatoana macho bure. Hakuna sababu ya kutoana macho, tunataka kugawanyika bila sababu,” alisema Nape. Alisema wapo watu walidhani kwamba katiba itakuwa njia fupi kwao kwenda Ikulu.
“Hupelekwi Ikulu na Katiba, unapelekwa Ikulu na kura za Watanzania,” alisema Nape bila kubainisha watu hao. Hata hivyo, katika Bunge Maalumu la Katiba, baadhi ya vyama vya upinzani, viliunda Umoja wa Katiba (Ukawa) ambao umeendelezwa hadi sasa na kuamua kushirikiana katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Nape alisema katika kuzunguka nchi nzima kupitia ziara hizo za Katibu Mkuu, Kinana, wamebaini Watanzania wanaipenda CCM. Hali inayohakikishia chama hicho kuendelea kuongoza nchi.
Akiendelea kusisitiza umoja wa kitaifa, Nape alisema wanaogombania idadi ya serikali kuingizwa kwenye katiba, wengi wanaangalia maslahi yao.
“Na ukiangalia sana, na hata hao wanaogombania mbili, tatu, nne kila mmoja anatafuta ulaji wake. Mwenye mbili anafikiria kuwa hii mbili nitapita, akiangalia akaona hakuna nafasi anasema tuongeze ya tatu na mimi nitapata sehemu fulani,” alisema.
Alisema watu hao hawapambani juu ya maslahi ya nchi. “Mwito wangu tutunze mshikamano,” alisema na kusisitiza wananchi kushikamana nakutatua matatizo yanayowakabili. Alisema yako mambo mengi ya kushughulikia kuliko kugombania katiba.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved