RC aitaka jamii kushiriki vita ajira kwa watoto

MKUU wa Mkoa Kigoma, Issa Machibya amesema kuwa tatizo la utumikishwaji wa watoto nchini halitakwisha kama jamii haitakuwa tayari kushiriki kikamilifu katika kupiga vita ajira za watoto.
Machibya alisema hayo mjini Kigoma katika maadhimisho ya Siku ya Watoto Duniani yaliyoandaliwa na asasi ya Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji (IRC) kupitia mradi wa WEKEZA ambao unatekelezwa mikoa ya Kigoma na Tanga ukihusisha kuokoa watoto kwenye mazingira hatarishi.
Alisema kuwa wapo watoto ambao wamekuwa wakitumikishwa kwenye kazi za mazingira magumu, ikiwemo kufanyishwa kazi za ndani, wakitumia muda mwingi na kupata muda mchache wa kupumzika.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa wapo viongozi waandamizi wa serikali, mashirika ya umma, taasisi za watu binafsi na watu binfasi ambao licha ya kushiriki katika kampeni hizo, lakini wamekuwa wakishindwa kuchukua hatua katika makazi yao ambapo vitendo hivyo vinafanyika.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za shirika la kazi duniani karibu asilimia 80 ya watoto wanaotumikishwa duniani wapo kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika ambapo hufanyishwa kazi kwenye maeneo ya vita, migodi, mashamba na uvuvi.
Awali akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Costantine Samari, Mratibu wa Mradi wa wekeza mkoa Kigoma alisema kuwa jumla ya watoto 5,041 wanaoishi kwenye mazingira magumu na hatarishi wamenufaika na mradi huo kwa kurudishwa shuleni na kupatiwa misaada mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved