Lukuvi amaliza mgogoro wa ardhi Chasimba, mwekezaji

HATIMAYE Serikali imekata mzizi wa fitina kwa kumaliza mgogoro wa ardhi wa muda mrefu uliokuwepo baina ya wakazi wa Chasimba na mwekezaji wa kiwanda cha saruji cha Wazo Hill, kwa kuirudisha ardhi hiyo kwa wananchi.
Hata hivyo, ardhi hiyo imerudishwa kwa wananchi hao ikiwa na masharti ambayo ni pamoja na kuachana na shughuli za uchimbaji wa chokaa, kokoto na mawe kutokana na eneo hilo lilipo kata ya Bunju na Wazo kubadilishwa matumizi na kuwa eneo la makazi kutoka eneo la madini.
Mgogoro huo umemalizwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ambaye alikuwa amefuatana na Mkurugenzi wa Kiwanda hicho, Alfonso Rodrudges na Mbunge wa Kawe Halima Mdee, ambapo alisema, licha ya ardhi hiyo kurudishwa kwa wananchi kuna mambo ambayo inabidi wananchi hao wayafuate vinginevyo, mpango huo utasitishwa.
Alisema wananchi hao wa maeneo ya Chasimba, Chatembo na Chachui walivamia hekta 243 za eneo la kiwanda hicho chenye hekta 922.55 lenye hati namba 42336, ambapo katika ya hekta hizo wananchi waliokuwa katika eneo la ekari 213 walikubali kufanyiwa tathmini kwa ajili ya kuondoka eneo hilo lakini waliokuwa kwenye hekta 30 walikataa na kukimbilia mahakamani.
“Serikali imekaa na huyu mwekezaji hapa na kufikia makubaliano, amesema haya mambo yanaweza kubaki kama yalivyo mkitaka na yanaweza kubadilika kama mkipenda, kuna watu wanataka kuona huu mgogoro ukiendelea, sasa msiruhusu hilo.
“Uamuzi wa serikali ni kuwa hatoki mtu hapa, ingawa ni lugha ya kujidai lakini ina masharti yake. Kwanza kichwani mjue kuwa kabla ya leo nyinyi mlikuwa ni wavamizi, lakini leo tumeamua kuwaondolea hadhi ya uvamizi na kuwa wamiliki,” alisema Lukuvi.
Hata hivyo alisema hadhi hiyo haiji bure, kwani wapo watu ambao walikuwepo wakati eneo hilo lilipofanyiwa tathmini kwa mara ya kwanza mwaka 2012, hivyo serikali itakaa na kukubaliana na watu hao.
Alisema lengo la kukaa na watu hao ambao picha zao zipo na nyaraka za kulipwa fidia kwa kipindi hicho ni kuepusha watu kutumia nafasi hiyo kujipenyeza na kupata viwanja katika maeneo hayo ambavyo vitakuwa vimepimwa.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved