Mchakato wa urais CCM waendelea kuunguruma.

KADA mwingine wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana alijitokeza kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa nafasi ya urais kwa chama hicho, katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu katika Mkao Makuu wa CCM mjini hapa, Dk Mussa Karokola, alisema kipaumbele chake ni kuinua uchumi na kupambana na walioshusha uchumi wa nchi kwa njia moja aunyingine.
“Mkakati wangu ni kuhakikisha uchumi unapanda, sitakuwa na huruma na watu ambao hawatalitelekeza hili, na pia wale waliochangia uchumi kutokuwa imara pia nitawashughulikia,” alisema.
Msanii Mwariko Wakati huo huo, Mtaalamu wa Sanaa za Kimataifa, Omar Athumani Mwariko, aliyechonga kifimbo kilichokuwa kinatumiwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, naye pia ametangaza nia ya kugombea uongozi huo wa juu nchini.
Mwariko ambaye ndio kwanza ametua nchini kutokea Marekani ambako amekuwa akifanyia shughuli zake za uchoraji, uchongaji na usanifu, amesema alishawishiwa na watu kadhaa, wakiwemo wasanii wenzake, ali arudi kugombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Ninatarajia kwenda mjini Dodoma kuchukua fomu za urais wiki ijayo,” alisema Mwariko na kuongeza kuwa akipata dhamana hiyo basi ataurejesha mfumo wa tawala za kiafrika kwa kuzitambua tena koo za machifu, watemi na Mangi ili kuwapa nafasi za uongozi. Kuhusu wagombea wengine waliojitokeza kuwania kiti hicho, msanii huyo anawaona kuwa hawana jipya maana walishakuwa kwenye uongozi na anadhani ni vyema Serikali ijayo iwe na sura mpya kabisa. Akizungumza jijini Arusha, Mwariko pia alionesha wasiwasi mkubwa na vyama vya upinzani vinavyounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Alijiunga na Chama Cha Tanganyika African National Union (TANU) mwaka 1974 na baadae kuhuisha uanachama wake CCM baada ya TANU kujiunga na Afro-Shirazi na kuunda Chama kipya 1977. Ana mpango wa kufufua Azimio la Arusha pamoja na kurejesha mfumo halisi wa uongozi wa kimila.
“Matatizo yetu mengi yanatokana na kuziacha mila na tamaduni zetu, sheria za kimila, pamoja na dawa za kienyeji bado zina nafasi kubwa sana katika nchi zetu za kiafrika na hususan Tanzania,” alisema Mwariko ambaye aliwahi kufanya utafiti wa miaka mitatu juu ya urithi wa asili kwa makabila ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved