WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya
amesema wingi wa wadhamini wanaojitokeza kudhamini wanaCCM wanaowania
kuteuliwa na chama chao kupeperusha bendera katika Uchaguzi Mkuu ujao,
wahamasishwe pia kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura.
Aidha, amewataka waliomwamini na kumdhamini, wengi wao wakiwa wasomi,
kutotishika na utitiri wa wagombea, wakiwemo wale wanaodhaminiwa na
maelfu ya watu, akisema hizo ni mbwembwe za kisiasa tu.
Mwandosya, mmoja wa wanaCCM zaidi ya 30 waliochukua fomu ya kuwania
nafasi hiyo, alisema hayo jana mjini hapa alipokuwa akizungumza na
wanaCCM wenzake waliojitokeza kumdhamini.
Katika siku ya jana wengi wa waliojitokeza kumdhanini Profesa
Mwandosya walikuwa ni wasomi wa Chuo cha Ushirika, lakini pia walikuwapo
mabalozi wa nyumba kumi pamoja na viongozi wa kata.
Profesa Mwandosya alionesha kufurahishwa baada ya kusikia kati ya
wadhamini wake kwa siku ya jana walikuwa ni wasomi na kusisitiza
wamemkumbusha alipokuwa akifundisha Chuo Kikuu.
“Msitishike na wanaodhaminiwa na watu 10,000 hizo ni mbwembwe za
kisiasa zisiwape shida, wadhamini wanaotakiwa ni 30 tu, hii ni zamu ya
udhamini tu ingawa zipo hisia, na hawa 10,000 wanatakiwa wahamasishwe
pia kujiandikisha na wahamasishwe pia kufanya kazi ya kujenga Taifa,”
alisema Profesa Mwandosya.
Aidha aliwashukuru wadhamini wake na kuwaahidi analo deni kubwa kwao
na atarehesha imani hiyo kwa kulitumikia Taifa kwa moyo na nguvu zake
zote.
No comments:
Post a Comment