WANACHAMA wa CCM wametakiwa kuwa macho katika uchaguzi wa viongozi
kwa kujihoji juu ya wanaotumia nguvu nyingi kusaka uongozi, wasije
kuchagua wanaojali maslahi binafsi.
Angalizo hilo lilitolewa juzi na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana kwenye mkutano wa hadhara mjini Biharamulo baada ya kuhitimisha
ziara ya siku 10 mkoani Kagera.
“Na ukiona mtu ana kimbelembele sana na anajifanya yeye ndiye anafaa,
mfikirie mara mbili. Huyo ana lake jambo…ukiona mtu usiku na mchana
anahangaika, huyo ana lengo lake,” alisema.
Akihutubia umati wa wananchi mjini hapa, Kinana aliendelea kusisitiza
wanaCCM wanapochagua mtu wasiangalie urafiki, ushabiki bali waangalie
kama wanayemchagua anajali maslahi yao na si yake binafsi.
Alisema wapo watu wengi wazuri kwenye jamii wanaofaa kugombea na
wananchi wanawataka, lakini hawako tayari kuingia kwenye kinyang’anyiro
kuhofia pilika zinazojitokeza katika siasa.
“Mtu ajipime, ukikaa kwenye jamii kuna watu wanaheshimika na
wanapendwa, lakini hawataki kuingia kwenye kashikashi za kutoa rushwa na
kukosewa heshima, lakini mtu ambaye hafai anajipeleka peleka ili
aonekane, waogopeni watu hao,” alisema Kinana.
Kinana ambaye alihimiza wana Biharamulo kuchagua CCM katika uchaguzi
mkuu mwaka huu tofauti na uchaguzi wa mwaka 2010 ambapo Chadema ndicho
kilishinda, alisema anaamini wakati mwingine, CCM inakosa kura kwa
sababu ya mikorogano ndani ya chama.
Awali, akizungumza katika kikao cha ndani cha chama, Kinana alisema
si lazima kila mmoja awe kiongozi. Alisema watu wengine wanasumbuliwa na
ulevi wa madaraka kiasi kwamba hawasikii lolote wanaloambiwa.
Katika hatua nyingine, Kinana alisema CCM kitaendelea kukemea
serikali inapokosea kwa kuwa wananchi wamekichagua na hawakuchagua
serikali. Alisema serikali anayoifahamu, ni mali ya wananchi.
Aliahidi kwamba ataendelea kunyoosha chama kiwe kinachojali maslahiya
wananchi. Alishutumu baadhi ya watumishi serikali wanaojigeuza miungu
watu kwa kuiba na kufanya ubadhirifu kwa kutegemea sheria iwalinde.
Alishutumu sheria ya Utumishi wa Umma akisema inalinda wabadhirifu.
Akihimiza wananchi kuchagua CCM, Kinana alisema wanajitahidi kurudisha
chama kwenye misingi yake.
Alisema CCM si malaika, kama ilivyo vyama vingine, wapo watu wa
hovyo. Katibu mkuu alisema ndani ya CCM, CUF, Chadema, NCCRMageuzi na
vyama vingine vya siasa, haikosekani kuwapo watu wa namna hiyo.
Alisema vitendo vya ulaji, wizi na rushwa havinarangi wala chama.
Hata hivyo alisema, chama kimeamua kusimamia na kurudisha misingi
iliyoasisiwa na waasisi wa taifa, ikiwa ni pamoja na kutenda haki na
kutetea wanyonge.
No comments:
Post a Comment