RAIS Jakaya Kikwete amesema siasa za nchi za nje na misingi mikuu ya
kuongoza mahusiano ya Tanzania na nchi za kigeni haitabadilika hata
baada ya yeye kuondoka madarakani baadaye mwaka huu.
Aidha, amewahakikishia viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika
(AU) kuwa yeye anaondoka madarakani, lakini Tanzania waliyoizoea na
kuijua itabakia pale pale na kuwaomba viongozi hao kumpa ushirikiano
mkubwa mrithi wake kama walivyompa yeye.
Alitoa uhakikisho huo mara mbili, juzi Jumapili wakati alipohutubia
kuwaaga wakuu wenzake wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) wakati
wa Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Umoja wa Afrika uliofunguliwa kwenye
Ukumbi wa Mikutano wa Sandton Convention mjini Johannesburg, Afrika
Kusini.
Wakati wa mkutano ujao wa kawaida wa AU mjini Addis Ababa, Ethiopia,
Januari mwakani, Tanzania itakuwa na Rais mpya, Rais wa Tano.
Aidha, Rais Kikwete alirudia kauli na msimamo huo wa Tanzania wakati
alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Somalia, Hassan Sheikh
Mahmoud ambapo kiongozi huyo wa Somalia amemjulisha Rais Kikwete kuwa
angependa kutembelea Tanzania baadaye mwaka huu.
Alisema Rais Kikwete kuwa misingi ya siasa za nchi za nje za Tanzania
na misingi mikuu ya kuongoza mahusiano yake na nchi za nje yaliwekwa
tangu Uhuru na hasa tangu kutungwa wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania
mwaka 1972 na tangu wakati huo haijapata kubadilika hata kama
wamebadilika viongozi mara nne sasa.
“Sina shaka kabisa kuwa misingi ya siasa za nje na misingi mikuu ya
uongozi wa nchi yetu itabakia ile ile isipokuwa kama Rais ajaye atatoka
chama kingine. Kitakachobadilika ni staili ya uongozi tu lakini misingi
ya uongozi itabakia pale pale kwa sababu ni misingi mizuri, ni misingi
ya busara ambayo imeongoza nchi yetu vizuri kwa miaka mingi.”
Aliongeza kusema: “Ni matumaini yangu kuwa Watanzania tutachagua
kiongozi mzuri atakayeendelea kutoa kipaumbele cha juu kwa masuala ya
Afrika pamoja na uanachama na ushiriki wetu katika Umoja wa Afrika. Hii
ni miongoni mwa misingi mikuu ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania tangu
uhuru mpaka sasa. Nawaomba mumpe ushirikiano mkubwa kama mlionipatia
mimi na hata kuzidi.”
No comments:
Post a Comment