WAZIRI wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wassira amesema yupo
tayari kumuunga mkono mgombea yeyote atakayeteuliwa na CCM kuwania urais
katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu, endapo nafasi hiyo
haitaangukia mikononi mwake.
Pamoja na ahadi hiyo, amesema hawezi kutoa jibu lolote kwa sasa kama
atagombea tena au hatagombea ubunge katika jimbo lake la Bunda kwani
haijaingia katika kinyang’anyiro hicho cha urais kwa ajili ya kushindwa.
Akizungumza na wanahabari kabla ya kukutana na wadhamini wake zaidi
ya 100 waliojitokeza kumdhamini mjini Iringa jana, Wassira alisema;
“mimi ni mtu mwenye uzoefu mkubwa wa kuongoza Watanzania, kwa hiyo
ninaamini nina fursa kubwa zaidi ya kuwa mgombea.”
Akizungumzia idadi kubwa ya wanaCCM wenzake wanaojitokeza kuwania
nafasi hiyo ya juu, alisema hashangazwi hata kidogo kwani CCM ina hazina
ya viongozi wengi wenye sifa za urais japokuwa katika hao waliojitokeza
hakuna anayemhofia.
“Tofauti na wale wenzetu, wao wana mtu mmoja mmoja tu katika vyama
vyao, ukizungumza CUF utamtaja Lipumba (Ibrahim) na vyama vingine ni
vivyo hivyo; ni sasa tu baada ya kuunganisha vyama vyao kupitia umoja
usio rasmi angalau unaweza kuona kama wako wengi, lakini kiuhalisia ni
wale wale wanaotegemewa na vyama vyao,” alisema.
No comments:
Post a Comment