Bunge imesifu juhudi za serikali za kutaka kuongeza fedha kwenye Mfuko wa
Umeme Vijijini (REA) kwa kupandisha bei ya petroli, dizeli na mafuta ya
taa, lakini ikaitaka serikali kuchukua tahadhari dhidi ya athari
zinazoweza kujitokeza kwa hatua hiyo.
“Kupeleka umeme vijijini kutaleta manufaa makubwa kwa wananchi kwani
kutachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii… lakini kwa kuwa tozo
zitakazokwenda kwenye mfuko zinatokana na mafuta na barabara, hatua hii
inaweza kusababisha gharama za maisha kupanda,” alisema Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Kidawa Salehe, bungeni mjini Dodoma
jana.
Makamu Mwenyekiti huyo alikuwa akiwasilisha bungeni Taarifa ya Kamati
yake kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2014, Mpango wa Maendeleo
wa Taifa kwa mwaka 2015/16, Tathmini ya Utekelezaji wa Bajeti ya
Serikali kwa mwaka 2014/15 pamoja na Bajeti ya Serikali 2015/16.
Katika bajeti ijayo, Serikali inapendekeza kuongeza tozo ya mafuta ya
dizeli kutoka Sh 50 kwa lita hadi Sh 100 kwa lita; petroli kutoka Sh 50
hadi Sh 100 kwa lita na mafuta ya taa kutoka sh 50 kwa lita hadi Sh
150.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Saluma alisema bungeni wiki iliyopita
kwamba Sh milioni 139.7 zitakazopatikana kutokana na ongezeko hilo
zitaelekezwa katika mfuko wa REA.
Kadhalika, alisema mafuta ya taa yameongezwa kodi ili kuondoa
uwezekano wa kuchakachua. Nayo bajeti mbadala iliyosomwa bungeni jana na
Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia, iliitaka serikali kufikiria upya
uamuzi wake wa kuongeza tozo kwenye mafuta.
Mbatia alisema nishati ya mafuta ni suala mtambuka linaloweza
kuongeza mfumuko wa bei na kusababisha ugumu zaidi wa maisha kwa
Watanzania.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, aliwakumbusha
wabunge wanaolalamikia tozo hiyo kwenye mafuta kwamba ilitokana na
wabunge wenyewe kupitia kamati mbalimbali.
No comments:
Post a Comment