MBUNGE wa Sengerema mkoani Mwanza, William Ngeleja |
Ngeleja alitangaza nia yake hiyo ya kuwania urais jana jijini Mwanza
katika Ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu (BoT) , akiwa ameongozana na baba
yake mzazi Mganga Ngeleja, mkewe Blandina na mtoto wa Shemeji yake Maria
Ntanga.
Sakata la Escrow na maadili
Alisema kuwa wakati wa Sakata la Escrow yeye alichafuliwa na baadhi
ya watu ingawa hakuweka bayana ni akina nani na kuongeza kuwa suala hilo
lilitolewa ufafanuzi na Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akizungumza na
wazee wa Dar es Salaam mapema mwaka jana.
“ Mimi katika suala la Escrow, Rais Kikwete alisema ni Sh bilioni 202
tu zilizobainika katika sakata la Escrow na kwamba zile hazikuwa fedha
za umma bali ni za kampuni binafsi, katika hili kuna watu kwa makusudi
wanaibua hasira za watu na kuwachafua wengine, wapo wanaotumia siasa
kuchafua watu,” alifafanua.
Kuhusu kuvuliwa wadhifa wa uwaziri kwa ajili ya kubainika katika
taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka
2012, alisema kuwa yeye hakuwa na kashfa kupitia ripoti hiyo na kamwe
hakuondolewa uwaziri kwa sababu ya kashfa bali aliondolewa katika
mabadiliko ya kawaida aliyoyafanya Rais Kikwete.
“Wapo watu wanaodhani katika mabadiliko ya mawaziri aliyoyafanya Rais
Kikwete Desemba 4 mwaka 2012, sikuwa na kashfa yoyote ile, yalikuwa ni
mabadiliko ya kawaida aliyoyafanya Rais Kikwete, hayakuwa ya kashfa
kutokana na ripoti ya CAG,” alisema na kuongeza.
“Ndio maana leo hii nasimama kwa kujiamini mbele yenu, kama mtu anao
ushahidi ajitokeze aseme hadharani kuwa mimi niliondolewa katika Baraza
la Mawaziri kwa kashfa,” alisema.
Aja na vipaumbele vinne
Alisema endapo atachaguliwa kuiongoza Tanzania, Serikali yake itakuwa
na vipaumbele vichache vinne vya kimkakati vitavyoiwezesha nchi iweze
kufanikiwa na kufikia malengo ya kuwa taifa lenye kipato cha kati.
Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni ujenzi wa uchumi imara, kuimarisha
utawala bora, kuboresha huduma za jamii (elimu, afya na maji) na
kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwemo ya reli, bandari,
barabara sanjari na kuiwezesha kuwa na umeme wa uhakika.
“Vipaumbele vyangu vikuu ni vinne, kujenga Uchumi imara; kipaumbele
namba mbili ni Utawala Bora; kipaumbele namba tatu ni Huduma za Jamii
(Elimu, Afya na Maji); kipaumbele namba nne ni Miundombinu kama reli,
bandari, barabara na umeme wa uhakika,” alisema .
No comments:
Post a Comment