RC Ndikilo awapa somo maofisa uandikishaji

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgbEgXqGXH9YTjDWyoWCgfcghuX0MFHD59oA24kgjo4XrPHld0W-PdcM5XWefpPoCxpdpQlZwquoK1POnjA1Fcm6Q0658aVO09QiXpnmnhK_NXjMKC3HZ4FzLiUZoIKZJVp2rz1ym07mkg/s1600/Evarist+Ndikilo..jpg
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, amewataka maofisa uandikishaji na uchaguzi wawe makini ili wasije wakaandikisha watu wasio na sifa ili uandikishaji huo usiharibike.
Aliyasema hayo jana mjini Kibaha wakati wa mafunzo kwa maofisa hao juu ya matumizi ya vifaa vya uandikishaji vya kielektroniki (BVR) wa mkoa huo na kusema kuwa baadhi ya watu ambao si raia wanaweza kutumia mwanya huo kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Ndikilo alisema kuwa kutokana na mkoa huo kuwa na bandari bubu nyingi ambazo zinaingiza raia wengi wa kigeni, baadhi ya watu wasio na sifa wanaweza kujiandikisha endapo hakutakuwa na umakini.
“Msipokuwa makini mnaweza kusababisha uandikishaji kuharibika kwani watu wasio raia hawastahili kujiandikisha kutokana na wao kutohusika katika zoezi la upigaji kura,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa watendaji hao wanapaswa kuhakikisha kuwa watu wote wenye sifa ambao ni raia wa Tanzania wa kuzaliwa au kuandikisha, kwa mujibu wa sheria wanapata fursa hiyo ili waweze kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba, mwaka huu.
“Vyama vya siasa havipaswi kuingilia kazi za maofisa waandikishaji, wanapaswa kuwepo kwenye vituo vya uandikishaji ili kufuatilia uandikishaji huo,” alisema Ndikilo.
Naye Ofisa Mchambuzi wa Kompyuta kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Mariam Rajab, alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwafundisha maofisa hao namna ya kutumia mashine hizo za BVR.
Rajab alisema kuwa changamoto kubwa waliyoiona kwenye baadhi ya maeneo ni watu wengi kujitokeza kuandikishwa na kwamba tayari vifaa vya kutosha vimepokelewa hivyo hakutakuwa na tatizo la uandikishaji.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved