Urasimu wakwamisha wakimbiza wawekezaji

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgHCEJ5Mts06Ozczc3iR8MqhkhLAm08qC0V6oQyoJczJur5L3tBNHm5lmftqmsbvc7POJ0xln4t0ddrk_RQUrnhKTW6Rp3xisbzHod7tVwZWcQgJACMt6UrEIychcVoKdlrtKw2sxm1DdjD/s1600/1.jpg
MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Godfrey Simbeye

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Godfrey Simbeye amesema kuwa urasimu mkubwa uliopo katika kusimamia masuala ya uwekekezaji umechangia kuwakimbiza wawekezaji.
Alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza katika Baraza la Biashara la Mkoa wa Kigoma. Alisema uchunguzi uliofanywa na taasisi yake umebaini Tanzania inapoteza fursa nyingi za uwekezaji kutoka nje ya nchi kutokana na mazingira ya urasimu na rushwa.
Simbeye alisema kuwa urasimu huo pia umekuwa ukilalamikiwa na Mabalozi wanaoiwakilisha nchi katika nchi mbalimbali ulimwengu ambao licha ya uhamasishaji mkubwa wanaoufanya, wameishia kupata lawama kutoka kwa wawekezaji waliofika Tanzania kutokana na urasimu waliokumbana nao.
Kutokana na hali hiyo, Simbeye alisema Tanzania imepoteza fursa nyingi za uwekezaji ambazo zingesaidia kukuza uchumi wa nchi kutoka hapa tulipo na kwamba Serikali inapaswa ichukue hatua madhubuti katika kukabiliana na hali hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mazingira ya Biashara kutoka Baraza la Taifa la Biashara nchini (TNBC), Arthur Mtafya alisema kuwa utititri wa kodi na tatizo la upatikanaji wa ardhi ni kikwazo kikubwa katika kuvutia wawekezaji nchini.
Mtafya alisema masuala hayo na urasimu wa vituo vya usimamizi wa masuala ya uwekezaji nchini, yanapaswa kuondolewa haraka ili kuweka mazingira ya kuvutia kwa uwekezaji na ufanyaji biashara usio na usumbufu ambao utawezesha kuinua uchumi wa nchi.
Akizungumza katika baraza hilo Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Mwanga mjini Kigoma, Raymond Ndabiyagese alisema kuwa kuwepo kwa Baraza la Biashara la Mkoa kutasaidia kuwaweka pamoja wafanyabiashara, serikali na taasisi mbalimbali zinazosimamia biashara ili kuzungumzia changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja.
Awali akifungua mkutano huo Mkuu wa Mkoa Kigoma, Issa Machibya aliwataka wakuu wa wilaya za mkoa huo kuhakikisha mabaraza ya biashara katika wilaya zao yanafanyika ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili kulingana na mazingira yanayowazunguka huku akibainisha umuhimu wa kuwepo kwa mabaraza ya biashara ya wilaya na mkoa kwa uchumi wa maeneo yao na taifa kwa jumla.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved