Serikali yaongeza mitambo ya kuzalisha umeme

http://www.ikulu.go.tz/files/gallery/ggggg_2.jpg
Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene

KUTOKANA na kukua kwa kasi ya mahitaji ya umeme, Serikali imeamua kuongeza mitambo mingine ya kuzalisha umeme kwa kiasi cha megawati 185 katika Mradi wa Kinyerezi I uliopo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene, alisema mitambo hiyo itasaidia kupunguza utegemezi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji ambayo huathiriwa na ukame, na mafuta ambayo ni ghali.
Akiwasilisha bajeti yake kwa mwaka 2015/16 bungeni juzi, Simbachawene alisema kazi zitakazofanyika ni kukamilisha usanifu wa mradi wa megawati 185 na kuajiri mshauri wa mradi.
"Fedha za ndani Sh bilioni 40 zimetengwa katika mwaka wa 2015/16 kwa ajili ya kuanza kutekeleza kazi hiyo," alisema Simbachawene.
Akizungumzia utekelezaji wa Mradi wa Kinyerezi I wa kuzalisha megawati 150, alisema umefikia asilimia 90. Alisema ufungaji wa mitambo ya kufua umeme kwa kutumia gesi asilimia umekamilika na ujenzi wa kituo cha kupozea umeme cha kilovoti 220/132 unaendelea.
"Kazi nyingine zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Kinyerezi hadi Kimara yenye umbali wa kilometa sana na ujenzi wa njia za kilometa tatu ya msongo wa kilovoti 132 hadi Gongo la Mboto," alisema na kuongeza: "Gharama za mradi ni Dola za Marekani milioni 183 na hadi sasa Serikali imetoa Dola za Marekani milioni 168, sawa na Sh bilioni 290.4.
Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2015." Katika maoni yao, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilisema pamoja na serikali kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Kinyerezi I, inaona kuna umuhimu wa kutafuta fedha zaidi kwa miradi ya Kinyerezi II, III na IV itakayozalisha megawati 870.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved