Mpango mpya kusimamia dawa, vifaa tiba wazinduliwa

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiAvHJlzr3ZnWFQMJut3Ib2Apmb12nGmU4kLyy6Knka0c81Z-rGE8aBnLJFkqKSjdPj7L5Fyh5IJQ3ZOf776ogxuYGTahlSev8Ivaf0CgxbEBSVsZVtQG26Rnd70rHxjMv_KEEcrVL-AUI/s1600/8.JPG
Waziri Wa Afya Na Ustawi Wa Jamii Dk. Seif Rashid

SERIKALI imezindua mpango wa kusimamia upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa njia za kielektroniki ili kuboresha na kumaliza manung’uniko ya watu kuhusiana na tatizo hilo.
Mpango huo uliozinduliwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Donald Mmbando mjini hapa unafadhiliwa na mashirika kadha ya kimataifa ikiwemo Shirika la Msaada la Marekani (USAID).
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mmbando alisema mpango huo unakuja kurekebisha mifumo ya awali ambayo ilikuwa inachelewesha maamuzi na kusababisha watu kukosa dawa.
Alisema Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya dawa, vifaa tiba na mawasiliano kiasi cha kufanya huduma Sekta ya Afya kuwa ngumu na ghali.
Alisema uzinduzi wa mfumo wa kutafuta, kuhifadhi na kutuma habari kwa njia ya mtandao utasaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma na hivyo kuiboresha Sekta ya Afya.
Alisema zipo halmashauri ambazo zimeonesha kwamba kukiwa na usimamizi wa karibu dawa haziwezi kukosekana na kusema kwa mfumo wa sasa inaonekana wazi kwamba hilo linawezekana.
Alizitaja halmashauri za Iramba, Meru na Rombo zimedhihirisha kuwa usimamizi wa karibu tu ndio dawa ya matumizi ya uhakika wa rasilimali fedha ikiambatana na makisio sahihi ya dawa.
“Mfumo mpya utamwezesha mtu akiwa ofisini kuomba dawa husika na kama amekosea mfumo utamwambia palepale na kama kituo cha jirani kina dawa ataelekezwa kuzifuata huko badala ya kuanza kugombana na Mganga wa Wilaya kumwandikia au kusubiri Bohari kumpatia dawa,” alisema.
Mfamasia wa Wizara na Mtaalamu wa Afya ya Jamii Edgar Basheka, alisema changamoto kubwa iliyokuwepo ni pamoja na ujazaji usio sahihi, ucheleweshaji kutokana na uhakiki na makisio yasiyo sahihi.
Alisema mpango huo ni sehemu ya mabadiliko yaliyofanywa na wizara ili kuweka utaratibu wa utoaji dawa, upatikanaji na mipango yake kuwa pamoja ili kurahisisha kazi na upatikanaji wa uhakika wa dawa kwa muda mfupi.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved