Upungufu wa maji Ziwa Tanganyika kudhibitiwa

Waziri Wa Maji Professa Jumanne Maghembe

SERIKALI ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wameanza kuchukua hatua za pamoja kukabiliana na kupungua kwa kina cha maji katika Ziwa Tanganyika kunakosababishwa na kubomoka kwa banio la Mto Lukuga uliopo DRC.
Mto huo unatoa maji kutoka Ziwa Tanganyika kupeleka Mto Kongo ambao unaenda kumwaga maji yake Bahari ya Atlantiki. Akizungumzia juhudi ambazo zinafanyika kulinda rasilimali maji ya Ziwa Tanganyika ambayo kwa sasa inaelekea kupungua na kusababisha matatizo,Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe (Pichani) alisema kwamba mikutano kadhaa imefanyika na tayari timu ya wataalamu imeundwa kuhusu ujenzi wa banio hilo na ulinzi wa rasilimali maji.
Alisema kwamba baada ya mkutano wa Aprili mwaka huu mjini Dodoma ulioazimia mataifa hayo mawili kushirikiana katika kulinda na kuendeleza rasilimali maji Ziwa Tanganyika kutokana na kuwa na asilimia 86 ya maji , misingi wa utekelezaji wa makubaliano iko tayari.
“Kuendelea kupungua kwa kina cha maji katika ziwa hilo kunafanya bandari za Kigoma upande wa Tanzania; na Kalemie, Uvira na Moba kwa upande wa DRC kuwa katika changamoto kubwa.”
Waziri Maghembe akisoma bajeti yake mjini Dodoma mwishoni mwa wiki alisema katika kukabiliana na changamoto hizo mkutano wa kwanza wa Mawaziri uliofanyika Aprili 16,2014, mjini Dodoma ulitoka na azimio la kushirikiana katika maeneo yanayohusu usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji za Bonde la Ziwa Tanganyika.
Hata hivyo alisema kabla ya kuanza utekelezaji wa makubaliano hayo, iliwalazimu kushughulikia kwanza masuala muhimu ili kuweka msingi wa utekelezaji, ambapo kila nchi ilitakiwa kuteua wataalamu watakaounda kamati ya pamoja ya kushughulikia mradi wa ujenzi wa banio la Mto Lukuga pamoja na masuala ya usimamizi wa rasilimali za maji.
Baada ya mkutano huo na ule uliofanyika Kalemie iliandaliwa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya mataifa hayo mawili kwa kuzingatia maeneo ya ushirikiano na sasa hati imesainiwa mwezi uliopita mjini Kinshasa Kongo na Wizara inajikita katika utekelezaji wa makubaliano.
Alisema katika mwaka wa fedha wa 2015/2016, Serikali ya Tanzania itaendelea kutekeleza shughuli zilizoainishwa kwenye MoU na pia kushirikiana kwa karibu na nchi za Burundi, Zambia na Sekretarieti ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved