Wizara ya Maji kuendelea kuondoa madini ya fluoride

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Jumanne Maghembe
WIZARA ya Maji imesema itaendelea kutekeleza mkakati wa kuondoa madini ya fluoride katika maji ya kunywa na kupikia kwa kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya kuondoa fluoride katika ngazi ya kaya .
Aidha imesema kwamba mitambo 1,000 ya kuondoa madini ya fluoride kwenye maji itasambazwa. Wizara hiyo pia imesema kwamba kazi ya kubaini vyanzo vya maji vilivyoathirika na madini ya fluoride itaendelea katika mikoa iliyopo kwenye ukanda wa fluoride.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe wakati akiwasilisha hotuba yake ya Wizara ya Maji mwishoni mwa wiki.
Hata hivyo Waziri Maghembe alisema katika ngazi ya jamii mitambo itajengwa kulingana na mahitaji. Alisema kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali, utafiti wa kupata mitambo ya kisasa yenye gharama nafuu utaendelea.
Pamoja na juhudi hizo, alisema Serikali inafanya maandalizi ya kupata benki ya takwimu na kuchora ramani inayoonesha maeneo yaliyoathiriwa na uwepo wa madini ya fluoride kwa wingi katika maji.
Hata hivyo alisema kwamba kazi iliyofanyika hadi sasa ni kutambua vyanzo vyote 38 vya maji katika halmashauri za wilaya za Arusha Mjini, Karatu, Arumeru, Longido, Monduli na Ngorongoro mkoani Arusha; Wilaya za Simanjiro, Hanang, Babati, Mbulu na Kiteto mkoani Manyara.
Alisema katika hotuba yake kwamba jumla ya vyanzo vya maji 954 vimekaguliwa na maji kufanyiwa uchunguzi wa kemikali na kuangalia uwepo wa madini ya fluoride.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved