KUSHUKA kwa kiwango cha uondoshaji mizigo bandarini kwa njia ya reli
kutoka asilimia 10 mwaka 2008 hadi kufikia asilimia moja hivi sasa,
kumeathiri uwezo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA)
kuweza kushindana kikamilifu na bandari za jirani.
Akitoa taarifa ya hali ya utendaji wa mamlaka hiyo kwa wahariri wa
vyombo vya habari nchini jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadhi
Massawe alisema utendaji hafifu na kuzorota kwa huduma za reli nchini
kumebakisha njia ya barabara kuwa tegemeo pekee kwa kusafirisha shehena
kutoka bandarini kwa asilimia 99 na gharama za usafiri huo kuwa wa juu
zaidi.
Alifafanua kwamba kudorora kwa uondoshaji wa mizigo kutoka Bandari ya
Dar es Salaam pia kumeathiriwa na msongamano wa magari katika barabara
za jiji, ubovu wa barabara zinazoingia na kutoka bandarini na zile
zinazounganisha bandari hiyo na maeneo ya kuhifadhia makasha.
Akizungumzia mafanikio ya mamlaka yake, Massawe alitaja kuwa ni
pamoja na kuongezeka kwa shehena iliyohudumiwa bandari ya Dar es Salaam
kutoka tani milioni 12 mwaka 2012/2013 hadi kufikia tani milioni 14.6
mwaka 2013/2014, upakuaji wa magari kuongezeka kutoka magari 671 kwa
shifti mwaka 2013 hadi kufikia magari 755 kwa shifti mwaka 2014, huku
muda wa meli kukaa bandarini kwa ajili ya kupakia au kupakua mizigo
kupungua kufikia siku 3.7 ikilinganishwa na lengo la siku 4 kwa mwaka
2014/2015.
No comments:
Post a Comment