MWANASIASA mkongwe nchini, Chrisant Mzindakaya na aliyekuwa mkuu wa
wilaya ya Sumbawanga, Kanali mstaafu Anthony Mzuri ambao ni wazee
maarufu mkoani Rukwa, wamemtambikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Tambiko hilo ni katika harakati zake za kuwania kuteuliwa na CCM kuwa mgombea wa chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.
Pamoja na tambiko hilo lililofanyika mjini hapa juzi, Pinda alisema
ana imani kubwa kuwa CCM kitatoa Rais ajaye mwenye sifa za uadilifu,
mwaminifu na mtetezi wa wanyonge.
Pinda alisema hayo wakati akiwashukuru wanachama wa CCM waliojitokeza
kumuunga mkono kwa kumdhamini katika kinyang’anyiro cha mbio za Urais
waliokusanyika katika ukumbi wa CCM uliopo katika uwanja wa Saba Saba
katika eneo la Izia mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, juzi.
Mkoani Rukwa wana CCM 1,896 waliojitokeza kumdhamini ambapo katika
wilaya ya Nkasi amedhaminiwa na wanachama 1,626 huku wilaya za
Sumbawanga Mjini na Sumbawanga Vijijini wamejitokeza wanachama 270
waliomdhamini.
Akiwa mkoani Katavi Pinda alidhaminiwa na watu 9,141. Akifafanua,
alisema ni faraja kwake kwani anaamini hakuna mgombea yeyote ambaye
amejaliwa kunong’ona na Mwenyezi Mungu licha ya kuwa kila mmoja wao ana
imani kuwa atakuwa yeye Rais ajaye.
Alitumia fursa hiyo kuwaaasa wagombea wenzake kuacha tabia ya
kutukanana , kuchafuana, kulalamikia bali wapendane kwa sababu mwisho wa
kinyang’anyiro hiki wote watakaoenguliwa hawana budi kuungana na
kumuunga mkono atakayependekezwa na Mkutano Mkuu wa CCM kupeperusha
bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
No comments:
Post a Comment