RAIA watatu wa China wamehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela au
kulipa faini ya Sh 300, 000 baada ya kupatikana na hatia ya kuishi
nchini na kufanya kazi bila kibali.
Washitakiwa hao waliohukumiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
ni Guo Chun Yang (44), Mi Yong (43) na Guo Jun Zang (43). Hakimu Mkazi
Waliarwande Lema alitoa hukumu hiyo jana baada ya washitakiwa kukiri
mashitaka yanayowakabili.
Awali Wakili kutoka Idara ya Uhamiaji, Method Kagoma alidai kuwa Juni
15, mwaka huu katika kituo cha mafuta cha GBP kilichopo Kawe,
Kinondoni, washitakiwa wakiwa raia wa China walikutwa wakiishi nchini
bila kibali.
Kagoma aliendelea kudai kuwa, washitakiwa walikutwa wakifanya kazi
bila kibali, aidha wanadaiwa kutotii amri halali iliyotolewa na
Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji.
Katika hatua nyingine, Raia wa Kenya Ian Kamau (27), alifikishwa
mahakamani hapo kwa tuhuma za kuishi na kufanya kazi nchini bila kibali.
Baada ya kusomewa mashitaka, mshitakiwa alikiri kuishi nchini bila
kibali na kukana kufanyakazi bila kibali.
Awali akisomewa mashitaka na Wakili kutoka Idara ya Uhamiaji
Celestine Makoba, alidaiwa Juni 15, mwaka huu katika ofisi za Uhamiaji
wilaya ya Ilala aliingia nchini bila kibali.
Aidha alidaiwa kujihusisha na biashara akiwa meneja wa kampuni ya
IENET Technologies bila kibali. Mshitakiwa aliachiwa kwa dhamana na kesi
imeahirishwa hali Julai 4 mpaka huu.
No comments:
Post a Comment