Lowassa awekwa mtu kati Monduli

WAKATI wakongwe wa siasa wakimhadharisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kutofuata mashabiki wanaomtaka ahame CCM ambako amelelewa na ndiko anakoheshimika, madiwani 20 wa chama hicho katika Jimbo la Monduli, wamejiunga na Chadema.
Madiwani hao wameingia Chadema na kufuatwa na wenyeviti sita wa vijiji pamoja na viongozi wa jumuiya za CCM, huku wakimwomba Lowassa ambaye ni Mbunge wa jimbo hilo, kufanya kinachoitwa ni uamuzi mgumu wa kuwafuata, baada ya CCM kukata jina lake sambamba na wagombea urais wengine 33, wakiwemo waliowahi kuwa mawaziri wakuu kama yeye.
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara, kabla ya kukabidhi kadi yake na za wenzake 19 wa CCM kwa viongozi wa Chadema, kiongozi wa Madiwani hao, Julius Kalanga kutoka Kata ya Lepurko, alisema wamefanya uamuzi aliouita mgumu, ambao Lowassa amekuwa akiuzungumza.
“Sisi tumeamua kujiunga Chadema kutafuta haki na kuondoka CCM ambako wanachakachua Katiba ya Chama kwa kumpitisha kiongozi wanayemtaka, badala ya kufuata Katiba na wananchi wanachotaka. “Tunamwomba Mheshimiwa wetu Lowassa, atufuate huku Chadema, afanye uamuzi mgumu aliokuwa akisema kila siku na asiogope kuhama… atakuwa amefanya uamuzi wenye tija kwa Taifa,” alisema Kalanga.
Diwani huyo pia aliwasihi wananchi kufuata madiwani wao wanakokwenda kwa sababu hata huko watachukua fomu na kugombea ili kuing’oa CCM madarakani.
Waliohama
Madiwani waliohama chama ni wa kata ya Engaruka, Engutoto, Esilalei, Loksale, Majengo, Makuyuni, Meserani, Nalalani, Lemooti, Moita, Monduli Juu, Monduli Mjini, Mferejini, Mswakini, Mto wa Mbu, Migungani, Selela, Sepeko na Lashaini.
Madiwani na viongozi hao ni Kalanga mwenyewe, Edward Lenanu, Bazir Siamini, Sigur Olekibinti, Loti Yamat, Goodluck Lerunya, Pashet Sengurumi, Yase Runja, Gidion Kimongishu, Dora Kipuyo, Mary Morindat, Sara Lomayan na Halima Lusinde.
Wengine ni Dotto Mlacha, Hawa Nyambiry, Alex Kamanda, Sion Kapela, Maria Lemta, Onesmo Naikoyo, Shaban Adam, Enditosidai Naikulo na Elifuraha Simon.
Pia yupo Dinna Solomon, Loti Naparana, Jocy Laizer, Edward Mathayo, Piniel Loning’o, Napir Mukare, Inot Leringa, Kalaine Lowassa, Maria Mepukori, Mary Stivin na Edward Kone.
Ushauri wa wakongwe
Mwito huo wa madiwani wa Monduli, unatofautiana na ushauri wa kada mkongwe wa CCM, Steven Mashishanga, aliyekaririwa akimtaka Lowassa atulie na aachane na ushawishi wa watu wanaomtaka ahame chama hicho.
Mashishanga katika mahojiano yake na gazeti moja la kila siku juzi, alimkumbusha Lowassa kuwa bado ni kiongozi anayeheshimiwa na jamii na kumuasa kuwa kama anahisi ameonewa, asamehe.
Akifafanua hoja zake, Mashishanga alisema wanaomshawishi Lowassa ahame CCM na wale wanaohama chama hicho kwa sababu ya kukatwa kwa jina la Lowassa katika kuwania urais, si wana CCM wa uhakika.
Kwa mujibu wa Mashishanga, ndani ya CCM mgombea akiteuliwa, wanachama huachana na yaliyopita na kuwa wamoja kwa ajili ya kukiendeleza chama.
Malaigwanani
Mbali na Mashishanga, pia wazee wa kimila wa jamii ya wafugaji wa Kimasai, maarufu malaigwanani kutoka Wilaya ya Monduli, nao wamemuomba Lowassa kuendelea kuwa kada wa CCM, kwa sababu ndicho chama kilichomlea na anakijua.
Mmoja wa malaigwanani, Mzee Joseph Mesopiro, kutoka Kata ya Sepeko, alikaririwa na vyombo vya habari kwa niaba ya malaigwanani akisema, wanakusudia kutuma ujumbe maalumu kwa Lowassa, utakaomshauri asihame CCM kama baadhi ya watu aliowaita wapambe wanavyomshauri.
Laigwanani mwingine, Julius Laizer kutoka Kata ya Moita, alisema bado anaamini kuwa CCM itaendelea kubaki imara, hata kama baadhi ya watu watakihama.
Lazier alisema viongozi waliolelewa na kukuzwa CCM, wanaamini chama hicho kitaendelea kuwa imara na hawako tayari kukubali ushawishi wowote wa kutaka wahamie upinzani.
Naye Mwenyekiti wa CCM Kata ya Lepurko wilayani Monduli, Njoput Alami, alikaririwa akibeza taarifa za kushawishi watu kuhama CCM kwa kisingizio cha Lowassa kukatwa katika majina ya wawania urais, akiziita ni kelele za wapambe wanaohofia kukosa fursa walizotarajia, iwapo Lowassa angeteuliwa kuwa mgombea urais wa CCM.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa aliwakaribisha na kusema Chadema watu wote wanapendana na hakuna ukubwa wala uongozi, hivyo wanapokuja huko ni kazi moja ya ukamanda kuwatumikia wananchi.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved