MSHAURI wa Ufundi wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars Abdallah
Kibadeni amesema hakutarajia kuona kiwango kikubwa cha soka kutoka kwa
wachezaji wa timu hiyo walipocheza na Uganda juzi.
Stars ililazimisha sare ya bao 1-1 na Uganda kwenye mechi ya kuwania
kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN)
iliyochezwa kwenye uwanja wa Nakivubo mjini hapa.
Kibadeni ameteuliwa kuwa mshauri wa timu hiyo chini ya kocha Charles
Mkwasa na Hemed Morocco. Wazawa hao walipewa mikoba ya kukinoa kikosi
hicho baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusitisha mkataba wake
na Mholanzi Mart Nooij baada ya kupata matokeo mabaya mfululizo.
“Mimi kwanza sikutarajia kiwango kikubwa kama hiki, maana kwanza
wachezaji wenyewe siwafahamu, lakini leo (juzi) nimeshuhudia mpira
mkubwa sana hapa,” alisema. Kibadeni ambaye enzi za ujana wake aliwahi
kuchezea klabu ya Simba na timu ya taifa alisema, timu iko vizuri la
muhimu ni kupewa muda na kuungwa mkono na Watanzania.
“Kwa hiyo Watanzania jamani wasiache kutuunga mkono, hii ni timu yao,
huu ni mwanzo tu, naamini tutafanya vizuri zaidi,” alisema. Baada ya
Mkwasa kupewa mikoba ya timu hiyo amefanya mabadiliko makubwa kwenye
timu, na mafanikio yake yameonekana katika mechi hiyo kwani timu
ilibadilika na kucheza kwa morali ya hali ya juu.
Matokeo hayo ya sare yameiondoa Stars kwenye kinyang’anyiro hicho
ambacho fainali zake zitafanyika mwakani mjini Kigali, Rwanda kwa jumla
ya mabao 4-1 baada ya kufungwa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza
iliyochezwa mjini Zanzibar wiki mbili zilizopita.
Aidha; kocha mkuu wa timu hiyo Charles Mkwasa aliwaomba Watanzania
kumpa muda zaidi ili aendelee kuinoa timu hiyo ambayo haijawahi kushinda
kwa muda mrefu huku akiridhishwa na kiwango kilichooneshwa na timu
yake.
Naye kocha wa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes Sredjovic Milutin
‘Micho’ aliimwagia sifa Stars na kukiri kuwa, kikosi chake kupata ugumu
dhidi ya wapinzani wake hao.
Mechi hiyo ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa
wachezaji wa ndani (CHAN), ilichezwa kwenye uwanja wa Nakivubo mjini
hapa na matokeo kuwa sare ya bao 1-1.
Micho alisema baada ya mchezo huo kuwa hakutarajia kupata upinzani
mkubwa katika mechi hiyo kama ilivyotokea. Katika mechi ya kwanza
iliyochezwa kwenye uwanja wa Amaan Zanzibar wiki mbili zilizopita,
Cranes ilishinda mabao 3-0 na kufanya kazi ya kusonga mbele kwenye
michuano hiyo kuwa rahisi kwao.
No comments:
Post a Comment