WABUNGE jana walipitisha Muswada wa Sheria ya Petroli wa Mwaka 2015,
ambao ni miongoni mwa miswaada ya sekta ya mafuta na gesi iliyokuwa
ikipigiwa kelele na wabunge wa upinzani.
Miswada mingine iliyokuwa ikipigiwa kelele, ambayo pamoja na huo wa
petroli iliwasilishwa kwa pamoja bungeni juzi ni Muswada wa Sheria ya
Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015 na Muswada wa Sheria
ya Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uchimbaji Tanzania wa Mwaka
2015.
Kutokana na hali hiyo wabunge zaidi ya 40 wa kambi ya upinzani kutoka
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walitolewa nje
ya Bunge Ijumaa na juzi kutokana na kufanya fujo wakati wa hatua za
kutaka kusomwa kwa miswada hiyo.
Baadhi ya wabunge hao wamefungiwa kuhudhuria vikao vyote vilivyobaki
vya Bunge hilo na baadhi wamesimamishwa kuhudhuria vikao viwili na
wengine vitano mfululizo.
Spika wa Bunge, Anna Makinda alisema muswada huo ulipitishwa kwa
kauli moja kwa wabunge kuitikia kwa kusema ndiyo, wakati waliosema
hapana hawakuwepo, hivyo sasa unasubiri Rais Jakaya Kikwete ausaini ili
uwe sheria.
Mbunge wa upinzani aliyekuwepo ni Hamad Rashid Mohammed (CUF-Wawi).
Miswada hiyo iliingia kwikwi kuwasilishwa bungeni baada ya semina ya
wabunge Jumanne iliyopita iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini
mjini hapa, ambapo wabunge wengi waliochangia siku hiyo waliomba
serikali isifanye haraka kuiwasilisha kwani muda hautoshi kujadili
masuala hayo nyeti.
Akichangia muswada wa mafuta kwa kujibu baadhi ya hoja za wabunge
jana, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage, alisema baadhi
ya watu wanapinga muswada huo kwa sababu unatoa nafasi ya asilimia 25
kwa kampuni ya Taifa, pia umeunda mamlaka ya udhibiti na pia hawapendi
ushiriki wa serikali katika masuala ya mafuta na gesi.
Akichangia hoja mapema jana kuhusiana na miswada hiyo, Mbunge wa Viti
Maalum, Martha Mlata (CCM), alisema kuna haja ya Watanzania kuwa makini
na kwamba gesi isijekuwa chanzo cha machafuko kama baadhi ya nchi.
Naye Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage alisema ni vyema kampuni za
mafuta na gesi zikalazimishwa na sheria kujiunga katika masoko ya hisa
hapa nchini ili kuwasaidia wananchi, badala ya kuachwa wawe katika
masoko ya hisa ya nchi wanazotoka.
Kwa upande wake wakati akiwasilisha maoni ya Kamati ya Nishati na
Madini juzi kuhusiana na muswada wa petroli, Mbunge wa Sumve, Richard
Ndassa (CCM), alisema serikali isikubali kufanyia marekebisho kifungu
cha 220 cha muswada huo.
Alisema kifungo hicho kilitolewa ushauri na Umoja wa Kampuni Kubwa za
Mafuta na Gesi (OGAT) kwa kupunguza masharti kuhusu kampuni ya nje
inayotaka kuwekeza kwenye utoaji wa huduma na bidhaa katika tasnia ya
mafuta na gesi asilia kushirikiana na kampuni ya Tanzania kwa ubia wa
asilimia 25.
“Moja ya hoja zao ni kwamba hakuna Mtanzania mwenye fedha za kutosha
kuwekeza kwenye tasnia ya mafuta na gesi asilia nchini kwa vigezo vya
uzoefu wa kimataifa wanavyotumia wao.
“Kamati haikubaliani na maoni hayo, kwani yanalenga kuwabagua
Watanzania kwa kuwajengea fikra za kushindwa hata kabla ya kuanza,”
alisema na kushauri serikali iimarishe mazingira ya kibiashara
kuwajengea uwezo wananchi wake waweze kushiriki katika fursa za
kiuchumi.
Pia alisema serikali ihakikishe inadhibiti kampuni bandia kutoka nje
ambazo zitajaribu kuonekana ni za hapa nchini. Wakati akiwasilisha
muswaada huo juzi, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene,
alisema unalenga kuondoa changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye
sera, sheria na miongozo mbalimbali ambayo ilikuwepo kwa muda mrefu ili
kuleta ufanisi bora zaidi katika sekta ya gesi asilia.
Alisema hatua hiyo ni kutoa fursa kwa Watanzania kushiriki katika
shughuli mbalimbali za kiuchumi/ kiuwekezaji katika sekta za mafuta na
gesi asilia nchini.
Alisema muswada huo unaanzisha taasisi tatu mpya ambazo ni Ofisi ya
Ushauri Kuhusu Petroli na Gesi chini ya Ofisi ya Rais, Kampuni ya Mafuta
ya Taifa na Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta
(PURA).
Wakati huohuo, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) na Mbunge
wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF) jana walitoka nje ya Bunge muda
mfupi baada ya kuomba mwongozo kwa Spika, Makinda wakidai
wamedhalilishwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyodai
walijutia kosa la kufanya fujo bungeni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti bungeni hapo, walidai hawakutoa
kauli hizo walipoitwa na kamati hiyo na kwamba hoja zilizotolewa na
kamati hiyo zilikuwa na lengo la kuwadhalilisha.
Hata hivyo Spika Makinda akijibu miongozo yao alisema ataenda
kujiridhisha kwa kuangalia hansad, ambapo baada ya majibishano na
wabunge hao waliinuka na kuamua kutoka nje ya Bunge.
Akizungumzia jambo hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Sera, Uratibu
na Bunge, Jenista Mhagama, alisema kama wabunge hao wanaona wameonewa
wakate rufani kwani taratibu ndiyo zinavyotaka.
No comments:
Post a Comment