SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), leo limeamua
kuwa, mchezaji Ramadhani Yahya Singano 'Messi' ni huru na sasa anaweza
kujiunga na timu yoyote.
Taarifa kutoka kwenye kikao cha Kamati ya Sheria Maadili na Hadhi za
Wachezaji ya TFF kilichofanyika leo, imesema kwamba Simba SC walishindwa
kutekeleza baadhi ya vipengele vya Mkataba, hivyo wanapoteza haki za
kummiliki mchezaji huyo.
Chini ya Mwenyekiti wake, Richard Sinamtwa, Kamati hiyo imejiridhisha
Messi hakuwahi kupewa nyuma ya kuishi na Simba SC jambo ambalo ni
kinyume cha Mkataba baina yake na klabu hiyo.
Simba SC iliwakilishwa
na Mwenyekiti wake wa Kamati yake ya Usajili, Zacharia Hans Poppe na
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Collins Frisch wakati Messi alifika na
Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Tanzania (SPUTANZA), Mussa Kisoky.
Maamuzi haya ni faraja kwa Messi ambaye anahusishwa kwa kiasi kikubwa
na kuhamia Azam FC. Messi aliyeibukia timu ya vijana ya Simba SC miaka
minne iliyopita, hivi karibuni ameibua shutuma dhidi ya klabu yake hiyo
kwamba imeghushi Mkataba wake. Messi anadai Mkataba wake halali ulikuwa
unamalizika mwaka huu, na si huu wa sasa ambao inaelezwa utamalizika
mwakani.
Lakini Simba SC imeendelea kusistiza mchezaji huyo alikuwa ana
Mkataba wa miaka mitatu. Awali, Sekretarieti ya TFF, chini ya Katibu
wake, Selestine Mwesigwa ilizikutanisha pande zote mbili, mchezaji na
Simba SC na kuamuru waketi chini na kutayarisha Mkataba mpya baada ya
kuona huu wa sasa una mushkeli. Hata hivyo, Messi akakataa na kuamua
kulihamishaia suala hilo Kamati ya Sheria ambayo leo imempa kile
alichotaka ‘kuwa mchezaji huru’.
Safari FIFA?; Hans Poppe amesema kwamba watakwenda mbele kusaka haki zao
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Hans Poppe amesema kuwa,
baada ya matokeo hayo, wanakwenda kukutana ili kujua hatua zaidi za
kuchukua, lakini dhahiri hawataishia hapo.
“Tuliwasilisha ushahidi
wote mbele ya Kamati, tumeonyesha mshahara wake ulikuwa kiasi gani na
tumeonyesha kwa nini alikuwa anapewa laki moja (100,000) zaidi.
Ili akalipie kodi ya nyumba, lakini bado hatukueleweka. Tunaamini
hapa si mwisho, vipo vyombo vingine ambavyo vitatupa haki yetu,
tunakwenda kukutana kuangalia uwezekano wa kulipeleka suala hili
huko,”amesema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ).
No comments:
Post a Comment