Tanzanite yachapwa na Zambia nyumbani

TIMU ya soka ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20, The Tanzanites, jana ilianza vibaya harakati zake za kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia baada ya kubugizwa bila huruma mabao 4-0 na Zambia katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.
Ni kipigo kizito kwa sasa Tanzanite inahitaji angalau ushindi wa kuanzia mabao 5-0 wakati timu hizo zitakaporudiana nchini Zambia baadaye.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ni miongoni mwa watu walioshuhudia kipigo hicho cha kusikitisha kutoka kwa wenzao wa Zambia The She-Polopolo.
Tanzanites inayofundishwa na mzalendo, Rogasian Kaijage ilizidiwa karibu kila idara na hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, walikuwa tayari walishapigwa 3-0.
Mabao ya Shepolopolo yaliwekwa kimiani na Memory Phiri dakika ya nne, Irene Lungu katika dakika ya 20 na Barbara Banda dakika ya 33.
Kipindi cha pili, Zambia iliingia uwanjani kwa nguvu na kupata bao la nne huku The Tanzanite wakionekana kuimarika kidogo baada ya kupata maelekezo kutoka kwa benchi la ufundi wakati wa mapumziko.
Wageni Zambia waliandika bao la nne dakika tano tangu kuanza kwa kipindi cha pili lililofungwa kwa penalti na Marry Wilombe. Mwamuzi Refa Batouli Ibrahim wa Sudan alitoa penalti hiyo baada ya Anastazia Anthony kumfanyia madhambi mshambuliaji wa Zambia, Memory Phiri.
Kikosi cha Tanzania; Najjiat Abbas, Zuwena Aziz, Happiness Hezron, Maimuna Hamisi, Anastazia Anthony, Donisia Daniel, Hamisa Athumani, Neema Paulo, Asha Shaaban Hamza/ Janet Cloudy (dk 40), Shelider Boniphace na Stumai Abdallah.
Zambia; Hezel Natasha Nali, Mary Wilombe/Osala Kaelo (dk 75), Margaret Belemu, Martha Tembo, Mlika Limwanya, Lwendo Chisamu, Esther Mukwasa, Irene Lungu, Grace Chanda, Barbara Banda na Memory Phiri/Agnes Musesa (dk 83).

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved