Lipumba aipasua kichwa CUF

  WANACHAMA wa Chama cha Wananchi (CUF) jana walimbana Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba wakimtaka kueleza ukweli juu ya taarifa zinazodai kuwa amejiuzulu wadhifa huo.
Wanachama hao walifika asubuhi na kukusanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya CUF Buguruni, Dar es Salaam, kwa lengo la kujua hatma ya kiongozi wao huyo. Walipofika hapo, alikuwa na kikao kirefu na wazee na viongozi wa dini kuhusu kile alichotaka kukieleza mbele ya vyombo vya habari. Baada ya kuwepo kwa kelele nyingi na za muda mrefu, zilizokuwa zikipigwa na wanachama hao zaidi ya 200, waliokuwa wakiimba nyimbo mbalimbali, ilimlazimu Profesa Lipumba kutoka ofisini kwake na kuwatuliza.
Hata hivyo, wanachama hao waliendelea kubaki na sintofahamu kutokana na yale aliyowaambia. Lipumba aliwataka wanachama hao, kuielewa vizuri Katiba ya CUF, kwa kuwa chama hicho kinaendeshwa kwa kufuata Katiba. Alieleza kuwa kila mwanachama kwa nafasi yake, anatakiwa kukijenga chama hicho.
“Mwaka 1995 nilikuwa ni mwanachama wa kawaida na niliteuliwa kuwa mgombea urais. Chama chetu ni taasisi, tena kubwa na sio mtu mmoja, hivyo tujenge chama chetu kama taasisi,” alisema Profesa Lipumba kisha kurudi ofisini kwake.
Hata hivyo, wanachama hao waliendelea kupiga kelele za kutaka ufafanuzi wa kauli hiyo, ambayo wengi walidai kuwa haijaeleweka inamaanisha nini. Mmoja wa viongozi wa dini, aliyejitambulisha kuwa ni Mchungaji Godfrey Sombi alisema hali si shwari, kwani Profesa Lipumba anataka kubaki mwanachama wa kawaida ndani ya chama hicho.
Mchungaji Sombi alisema sababu kubwa ni kutokana na baadhi ya viongozi wa Umoja wa vyama vinne vya upinzani (Ukawa), ambao chama hicho ni miongoni mwa vinavyounda umoja huo, kuvunja malengo yake.
“Hajaridhishwa na ujio wa Lowassa (Edward) ndani ya Ukawa na kupewa nafasi ya kupeperusha bendera kwa nafasi ya urais, kwa hiyo anataka kubaki kuwa mwanachama wa kawaida,” alisema kiongozi huyo wa dini.
Lowassa amejiunga na Ukawa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wiki moja iliyopita na juzi aliteuliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho na umoja huo, wenye vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanachama wa CUF walimtaka Profesa Lipumba kuweka wazi kuhusu taarifa zinaripotiwa na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Walitaka Profesa huyo maarufu wa Uchumi na aliyegombea urais mara nne tangu mwaka 1995, aendelee kuwa kiongozi wao, kwani wana imani naye. Abdallah Simba alisema kauli iliyotolewa na Profesa Lipumba, bado imewafumba macho, kwani hawaelewi ukweli wa taarifa za kujiuzulu na walitegemea angetoa taarifa za kukanusha kujiuzulu ndani ya chama hicho au kueleza kinachoendelea.
Kwa upande wake, Hamis Issa alisema wao kama wanachama, hawataki suala la kujiuzulu kwa Profesa Lipumba litokee, kwani wanaamini ni kiongozi mwenye uwezo mkubwa anayeweza kuwafikisha mbali zaidi.
Awali, Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya alisema mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Profesa Lipumba, umeahirishwa mpaka siku nyingine kutokana na mwenyekiti wao kuwa na kikao na wazee na viongozi wa dini.
“Mwenyekiti ndiyo aliwaita alitaka kuzungumza na ninyi yaliyo moyoni mwake, lakini asubuhi amevamiwa na wazee na wanachama katika ofisi yake, wazee wanataka kujua yanayoendelea.
Hata mimi mwenyewe sijui alikuwa anataka kuzungumza nini ndio kuna hicho kikao wazee wanataka kujua alikuwa anataka kusema nini na vyombo vya habari,” alisema Sakaya.
Wakati wote wakati kikao kati ya Profesa Lipumba na wazee kikiendelea, wanachama hao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za chama na kumsifu huku wakitaka aje kuzungumza nao.
Wakati Profesa Lipumba akiondoka katika ofisi hizo, wanachama hao walitaka gari lake ambalo wakati huo halikuwa na bendera ya chama hicho kikuu cha zamani cha upinzani nchini, liwekwe bendera kuashiria ni gari la kiongozi wa chama.
Tangu Lowassa aruhusiwe kujiunga na Ukawa na baadaye Chadema, kumeibuka mgawanyiko ndani ya Chadema na sasa CUF, baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kujiweka kando akipinga Waziri Mkuu huyo wa zamani waliyemtangaza kwa miaka saba kuwa fisadi, kujiunga nao na kuwa mgombea urais.
Profesa Lipumba alikuwapo wakati Ukawa ikitangaza kumkaribisha katika umoja wao, na pia wakati Chadema ikimtangaza kuwa mwanachama wao. Lakini, baadaye alianza kukosekana katika matukio muhimu ya umoja huo.
Juzi hakuwapo wakati Lowassa akipitishwa na Mkutano Mkuu wa Chadema kuwa mgombea urais pamoja na Mgombea Mwenza, Juma Duni Haji ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF Zanzibar na sasa amehamia Chadema.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad alihudhuria mkutano huo, uliofanyika Dar es Salaam na alitangazwa kuwa Mgombea wa Urais wa Ukawa kwa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved