Chama kipya cha siasa chapata usajili wa muda

Msajili wa vyama vya siasa Tanzania Jaji Francis Mutungi
MSAJILI wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi jana alikabidhi cheti cha usajili wa muda kwa chama kipya cha siasa cha Maadili na Uwajibikaji (CM-TANZANIA).
CM-TANZANIA ni chama cha 23 kupokea usajili baada ya vyama vingine vya siasa 22 vyenye usajili wa kudumu.
Akikabidhi cheti hicho Dar es Salaam jana, Jaji Mutungi aliviasa vyama vya siasa nchini kuepukana na migogoro na kutumia vikao vyao katika kuendeleza shughuli zao za kisiasa.
Aidha, Jaji Mutungi amevitaka vyama vya siasa nchini kufanya siasa na sio uanaharakati kwani kwa kufanya hivyo malengo yao yatatimia na kuifanya Tanzania kuwa na amani.
“Msipende kukimbilia kwenye vyombo vya habari mnapokuwa na migogoro, bali malizeni tofauti zenu ndani ya vikao vyenu kulingana na Katiba ya vyama vyenu,” alisema Jaji Mutungi.
Aliongeza kuwa Tanzania inapaswa kuwa na vyama vya siasa vinavyojitambua na vinavyojua wajibu wao katika kuleta maendeleo ya Taifa kwani siasa sio chuki wala uhasama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Maadili na Uwajibikaji (CM-TANZANIA), Laban Nkembo alisema chama hicho kimeanzishwa kwa lengo la kuiweka Tanzania kimaadili na uwajibikaji kwa kuwa kinabeba mambo makubwa mawili yakiwemo amani na upendo.
Aliongeza kuwa chama chao sio cha upinzani na kinaheshimu chama kilichopo madarakani hivyo, kinaahidi kushirikiana na chama tawala kuenzi mazuri yanayofanywa na chama hicho.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved