Mafanikio ya Jeshi la Afghanistani dhidi ya Daesh

 
Sambamba na sisitizo la viongozi wa serikali ya Afghanistan katika kukabiliana na magaidi, makamanda wa jeshi wametangaza kusambaratisha ngome kuu ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika wilaya ya Achin mkoani Nangarhar, mashariki mwa nchi hiyo.
Zaman Waziri, mmoja wa makamanda wa jeshi la Afghanistan sanjari na kutangaza habari hiyo, amesema kuwa hivi sasa maeneo mengi ya mkoa huo yako chini ya udhibiti wa askari wa serikali. Fazal Ahmad Shirzad, kamanda wa polisi katika mkoa wa Nangarhar amesema kuwa, katika operesheni dhidi ya magaidi wa kundi la Daesh, askari wa serikali wamewatia hasara kubwa wanachama wa kundi hilo. Aidha kamanda huyo wa polisi amewataka wakazi wa mji wa Achin waliokuwa wamekimbia makazi yao ili kuokoa maisha yao, warejee makwao na kuendelea na maisha yao ya kawaida ingawa pia amewataka washirikiane na maafisa usalama wa seikali dhidi ya magenge ya kigaidi. Kwa mujibu wa viongozi wa eneo hilo, jeshi na askari polisi nchini Afghanistan, wamekuwa wakikabiliana na wanachama wa genge la kigaidi la Daesh kwa kipindi cha miezi minane sasa katika wilaya ya Achin mkoani Nangarhar, mashariki mwa nchi hiyo. Hivi sasa operesheni za kukabiliana na wanachama wa genge hilo, zingali zinaendelea katika kuzisafisha wilaya nne nyingine za mkoa wa Nangarhar nchini humo. Maafisa wa seikali wametangaza pia kwamba katika operesheni za kuusafisha mji wa Achin kutoka mikononi mwa genge hilo, askari wa serikali wamefanikiwa kudhibiti kiasi kikubwa cha silaha na zana za vita zilizokuwa zikitumiwa na magaidi hao. Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh lilikuwa linajaribu kuudhibiti mkoa wa Nangarhar ili kuubadilisha kuwa ngome yao kuu nchini Afghanistan. Hata hivyo njama hizo zimefeli baada ya kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa jeshi la nchi hiyo. Kwa mujibu wa baadhi ya duru za usalama, jeshi la Afghanistan lilianzisha operesheni kali za kuutwaa mji wa Achin kuanzia tarehe 16 ya mwezi huu wa Februari. Kwa upande wake msemaji wa jeshi la polisi mkoani Nangarhar, Hazrat Hussain Mashriqwal, amesema kuwa katika operesheni hiyo magaidi 50 wa Daesh wameangamizwa. Kwa mujibu wa afisa huyo wa jeshi la polisi, wakazi wa mkoa huo walishirikiana bega kwa bega na askari dhidi ya matakfiri hayo maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya binaadamu. Hayo yanajiri katika hali ambayo, katika mwendelezo wa mafanikio ya serikali ya Kabul dhidi ya magaidi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan imetangaza kuwa, imefanikiwa kumtia mbaroni mmoja wa makamanda muhimu wa kundi la kigaidi la Taleban katika mkoa wa Ghor. Gaidi huyo anayeitwa Mawlawi Abdur-Rahman, alinaswa kupitia operesheni maalumu za askari wa polisi katika viunga vya wilaya ya Firuzkuh mkoani Ghor, katikati mwa nchi hiyo. Ripoti za awali zinaeleza kuwa, gaidi huyo alikuwa mratibu wa hujuma za kigaidi katika mkoa huo. Aidha Wizara ya Mambo ya ndani ya Afghanistan imewasisitizia wananchi kuwa jeshi la polisi liko macho na kwamba halitaruhusu maadui kuvuruga usalama wao. Wakati huohuo, wakazi wa miji kadhaa ikiwemo Kabul, mji mkuu wa nchi hiyo sanjari na kufanya maandamano makubwa ya kulaani mashambulizi ya kigaidi, wameitaka serikali kukabiliana vikali na kundi la Taleban na makundi mengine ya kigaidi yanayovuruga usalama wa nchi yao. Washiriki wa maandamano hayo, sanjari na kuunga mkono vikosi vya usalama vya nchi hiyo, wametangaza utayarifu wao kwa ajili ya kukabiliana na magenge hayo ya kigaidi. Ala kulli hal, kusambaratishwa ngome kuu ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika wilaya ya Achin mkoani Nangarhar kunatajwa na weledi wa mambo kuwa hatua moja mbele katika mafanikio dhidi ya makundi ya kigaidi ambayo hivi sasa yanataka kujizatiti katika nchi za Asia ya Kusini na Kati.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved