Mtoto wa miaka minne jela kwa mauaji huko Misri

Mtoto wa miaka 4 jela maisha kwa mauaji Misri!!Mahakama moja nchini Misri imemUhukumu kifungo cha maisha jela mtoto mmoja wa miaka 4 kwa tuhuma za kufanya mauaji akiwa na umri wa baina ya mwaka mmoja na miwili.
Kwa mujibu wa toleo la mtandaoni la gazeti la New Vision la nchini Uganda, Ahmed Mansour Karmi amepatikana na hatia ya mashtaka manne ya mauaji, manane ya jaribio la mauaji, shitaka moja la wizi wa kutumia mabavu na jingine la kuwatishia maisha askari na maafisa wa polisi wa nchi hiyo, yote hayo akidaiwa kufanya kabla ya kutimiza umri wa miaka miwili. Ahmed ambaye hakuwa kortini wakati wa hukumu hiyo, ni mmoja kati ya watuhumiwa 115 ambao wamehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa tuhuma za kuhusika na jinai zilizofanywa nchini Misri mapema mwaka 2014. Faisal al-Sayd, wakili wa mtoto huyo amesema kuwa jina la mtoto huyo liliongezwa kwenye orodha ya watuhumiwa kimakosa na kwamba mahakama haikumkabidhi jaji aliyetoa hukumu hiyo, cheti cha kuzaliwa cha mtoto huyo, ili kuhakikisha kuwa alizaliwa Septemba mwaka 2012 au la. Wakili huyo amesema licha ya kukabidhi cheti hicho, lakini mahakama hiyo iliipeleka kesi hiyo katika mahakama ya kijeshi ambapo mtoto huyo alihukumiwa pamoja na watuhumiwa wengine 114. Mwanasheria huyo ambaye alikuwa akizungumza kwa hasira amesema: “Hii inadhihirisha kuwa jaji hakuisoma wala kuitafakari kesi iliyokuwa mbele yake na huu ni ushahidi kwamba hakuna haki nchini Misri.” Ni vyema kuashiria hapa kuwa, zaidi ya wanachama 40,000 wa upinzani wakiwemo wafuasi wa Ikhwanul Muslimin wanazuiliwa katika mazingira ya kutisha katika korokoro za nchini Misri pasina na kufanya kosa lolote. Itakumbukwa kuwa, mwezi Julai mwaka 2013 jeshi la Misri likiongozwa na Jenerali Abdul Fattah al-Sisi lilimpindua Muhammad Morsi, rais wa kwanza kuwahi kuchaguliwa kidemokrasia katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved