Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), imesema Kampuni ya StarTimes inayouza
ving’amuzi kwa ajili ya ‘chaneli’ mbalimbali za televisheni, ikiwamo
Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) inafanya biashara ya simu kupitia
mgongo wa mtu.
Hilo
limebainika katika uchunguzi unaofanywa na TRA dhidi ya kampuni hiyo,
kufuatia maboksi 294 yaliyokamatwa yakiwa na simu 2,744 na vifaa vyake
ndani ya ghala lake mwezi uliopita.
Akizungumza
jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Walipakodi, Richard Kayombo
alisema uchunguzi unaoendelea kufanywa umebaini kuwa maboksi hayo
yalikuwa ya StarTimes, tofauti na taarifa za nyaraka za mizigo
zilivyokuwa zikieleza kuwa mizigo ni ya mtu mwingine.
“Tulifuatilia
tukabaini hii biashara ambayo wanaifanya Startimes wanamtumia mtu
mwingine kama sehemu ya kukwepa kodi, kwani nyaraka zilionyesha mzigo ni
wa mtu mwingine, lakini katika kuchunguza tumebaini ni wa StarTimes,” alisema Kayombo.
Alisema
wanaendelea na uchunguzi zaidi ili kujua kama biashara hiyo inayotumia
jina la mtu imekuwa ikifanywa kwa muda gani, lakini pia wanaendelea
kufanya utaratibu wa kampuni hiyo kulipa kodi ya mizigo hiyo.
“Bado
tunafanya taratibu za namna ya kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria,
ikiwa ni pamoja na kulipa kodi ambayo ilitakiwa ya Sh118 milioni,” alisema.
Mwenyekiti
wa bodi ya StarTimes, Clement Mshana alipotafutwa kuzungumzia suala
hilo alisema maswali hayo aulizwe Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo,
Lanfang Liao huku akisisitiza hana taarifa za kina kuhusu ripoti hiyo.
“Mwambie
akufahamishe zaidi huyo ndiye mtendaji mkuu wa kampuni. Hata hivyo hiyo
stori inayomkariri mtu wa TRA sijaisoma hivyo sina taarifa za kina juu
ya alichoeleza TRA,” alisema.
Hata
hivyo, alipoombwa namba yake ya simu hakuwa tayari kutoa, badala yake
alituma ujumbe wa maneno uliosema kuwa “nimemwambia ofisa uhusiano
atakupigia”.
No comments:
Post a Comment