Mauaji
ya kikatili ya Diwani wa Kata ya Kimwani, Wilaya ya Muleba mkoani
Kagera, Sylvester Muliga (CUF), yameanza kuibua mambo mazito huku
ikielezwa kuwa Ijumaa alikuwa awasilishe hoja kwenye Baraza la Madiwani
kuhusu masuala ya ardhi.
Muliga
ambaye alifia Hospitali ya Kagondo alikopelekwa kwa matibabu baada ya
kukatwa mapanga Jumapili usiku, imeelezwa kuwa katika kikao hicho
ilikuwa aombe kuundwa kwa kamati ya kuchunguza uhalali wa maeneo makubwa
ya ardhi yanayomilikiwa na watu wachache.
Kwa
mujibu wa mjumbe wa Kamati ya Uchumi na Mazingira ambaye pia ni Diwani
wa Kata ya Kasharunga, Khalid Swalehe, hoja hiyo ilikuwa iwasilishwe na
Muliga na ilikuwa inaungwa mkono na madiwani wa kata zote zilizo na
migogoro ya ardhi.
Baada
ya taarifa za kufariki dunia kwa diwani huyo, wananchi walivamia nyumba
nane za watuhumiwa wanaodaiwa kutekeleza mauaji hayo na kuziteketeza
kwa moto.
Pia, walichoma moto mashine mbili za kusaga na kuharibu gari la mmoja wa wagombea wa udiwani katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kyota, Daudi Kiruma, wananchi wamehusisha mauaji hayo na mambo ya siasa.
“Kinachoonekana hapa baadhi ya watu wanataka kupotosha ajenda ili wahusika wa mauaji wapate nafasi ya kutoroka,” alisema Kiruma.
Hata hivyo, Kiruma alisema hana uhakika kama mtuhumiwa anayedaiwa alikuwa mgombea amekamatwa, kwa sababu haonekani.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, jana alisema wanamshikilia
mtuhumiwa mwingine ambaye anafanya idadi ya walikomatwa kuhusiana na
mauaji hayo kufikia watatu mpaka sasa.
No comments:
Post a Comment