Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.
Mohamed Othman Chande amesema kuwa Mahakama ya Tanzania itawachukulia
hatua za kinidhamu na za kisheria Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo,Wilaya
na wale wa Mahakama za Hakimu Mkazi wapato 508 kote nchini waliotekeleza
majukumu yao chini ya kiwango na kushindwa kutimiza wajibu wa Mahakama
wa Utoaji wa Huduma Bora kwa wananchi katika mwaka wa Sheria wa
2015/2016.
Akizungumza na waandishi wa
Habari leo jijini Dar es salaam alipokua akitoa ufafanuzi kuhusu kuanza
kwa mwaka mpya wa Sheria wa 2016 na Maadhimisho ya Wiki ya Sheria
ambayo kilele chake kitakua Januari 4,2016 Jaji Mkuu amesema kuwa kwa
mujibu wa taratibu za uendeshaji wa Mahakama na upimaji wa viwango vya
utendaji kazi vilivyowekwa, Mahakimu hao wa Mahakama za wilaya na Hakimu
Mkazi 121 na 387 wa Mahakama za Mwanzo watatakiwa kutoa maelezo ndani
ya siku 7 juu ya sababu zilizowafanya washindwe kutimiza lengo
lililowekwa la kushughulikia mashauri 260 kila mmoja.
Amesema watakaothibitika kamati
za nidhamu na maadili za kila wilaya na Mikoa ambazo ni Kamati ndogo za
Tume ya Utumishi wa Mahakama zitawafungulia kesi za kinidhamu ndani ya
siku 21.
“Wale watakaobainika watakumbwa
na adhabu ya kupewa Onyo, kushushwa vyeo na kufukuzwa kazi ili iwe
fundisho kwa wengine, ninajua wapo baadhi ambao waliajiliwa katikati ya
mwaka, wengine kwenda mafunzo ya vitendo vyuoni, wajawazito na baadhi
vituo vyao kuwa na kesi chini ya 260 kwa mwaka” Amesisitiza.
Aidha, katika hatua hiyo
amewapongeza Mahakimu waliofanya vizuri katika utendaji wao wakiwemo 14
walioshughulikia mashauri zaidi ya 700 kila mmoja, Mahakimu 50 walioamua
kesi zaidi ya 500 kila mmoja baadhi wakitokea wilaya ya Mkuranga,
Rufiji na Bukoba mjini na wengine wawili kutoka Dar es salaam walioamua
kesi zaidi ya 900 kila mmoja na kuvuka lengo la utendaji lililowekwa
la kushughulikia mashauri 260 kwa mwaka.
Akitoa tathmini ya utendaji wa
Mahakama kwa mwaka wa sheria uliopita amesema kuwa Mahakama ya Tanzania
ina Mahakama za Hakimu Mkazi kila Mkoa na Mahakama za Wilaya 111 katika
wilaya za Kiserikali 133 pamoja na Mahakama za Mwanzo ambazo hupokea
asilimia 93 ya mashauri yanayofunguliwa kote nchini.
Amesema mwaka 2015 Mahakama zote
nchini zilipokea jumla ya mashauri 206,115, kati ya hayo mashauri
220,815 yaliamuliwa kukiwa na ziada ya mashauri 14700 jambo
linaloonyesha kuwa Mahakama zinapokea mashauri na kuyashughulikia kwa
kasi inayoridhisha huku mashauri yanayosababisha mrundikano ni yale
yaliyo nje ya idadi iliyopangwa.
Ameongeza kuwa katika katika
kipindi cha mwaka huo wa 2015 Mahakama za Mwanzo zilipokea mashauri
141,025 ambapo kati ya hayo Mashauri 149,757 yalishughulikiwa huku idadi
ya Mahakimu walioshughulikia mashauri hayo ni 1240.
“Ukiangalia mwenendo wa ufunguaji
wa mashauri yote kote nchini hasa Tanzania Bara utagundua kuwa Mahakama
za Mwanzo, Wilaya na zile za Hakimu Mkazi zinapokea mashauri mengi kwa
asilimia 93 ,katika kila mashauri 4 yanayofunguliwa nchini 3 yako
mahakama za mwanzo ambako wananchi wengi wanatafuta ufumbuzi wa kesi zao
lazima tuweke mkazo” Amesema Jaji Mkuu.
Kuhusu kuanza kwa mwaka mpya wa
Sheria mwaka 2016 amesema Mahakama inauanza chini ya Kauli Mbiu Isemayo
“Huduma Bora kwa Wananchi ni Wajibu wa Mahakama na Wadau wake” ikiwa na
kesi 20,431 ikilinganishwa na 34,126 ilizoanza nazo mwaka 2015 na
kuongeza kuwa licha ya changamoto zinazoikabili Mahakama ya Tanzania
mkakati uliopo ni kupunguza idadi hiyo hadi kufikia 0 kwa kila mwanzo wa
mwaka wa sheria.
Akitoa ufafanuzi kuhusu
upatikanaji wa Nakala za hukumu amesema Serikali inaendelea kuijengea
uwezo wa kifedha Mahakama wa kuajiri wachapaji wa nakala wengi zaidi ili
Nakala za Hukumu za Kesi ziweze kupatikana pindi tu kesi zinapomalizika
katika mahakama zote nchini tofauti na ilivyo sasa ambapo hupatikana
Mahakama Kuu na Mahakama za Rufani.
Aidha, amesema Mahakama
inaendelea kuboresha miundombinu yake ikiwemo majengo na ujenzi wa
mahakama mpya katika maeneo yasiyo na huduma hiyo katika mwaka 2016. “
Hivi sasa tuna wilaya 23 hazina Majengo ya Mahakama za wilaya, kwenye
baadhi ya maeneo kesi zinasikiliziwa Ofisini kwa Hakimu wakati ilitakiwa
ziwe kwenye jengo lenye ukumbi wa wazi,tumejiandaa kwa michoro ya
majengo kwa mahakama zote ili tuanze kujenga kwa gharama nafuu”
Mhe. Chande ametoa wito kwa
wananchi kutosita kuitumia Mahakama ya Tanzania katika kupata ushauri wa
kisheria kupitia wataalamu wake, kuhudhuria maonesho mbalimbali ya
kisheria yanayofanyika nchini huku akitoa angalizo kwa baadhi ya watu
wanaochangia kuwepo kwa mrundikano wa kesi kwa kufungua kesi za madai au
kupeleka mashauri Mahakamani kama sehemu ya maegesho ya masuala yao.
“Baadhi ya watu wamekuwa
wakipeleka kesi Mahakamani kama sehemu ya maegesho, huzifungua kisha
hushindwa kujitokeza Mahakamani hizi ni tofauti na zile zenye vipengele
vingi ndani ya kesi moja au zile ambazo mashahidi wake wamehama kutoka
eneo moja kwenda linguine, hizi nawahakikishia tutazifuta ili kupunguza
mrundikano wa kesi kwenye Mahakama zetu” Amesisitiza Mhe. Chande.
No comments:
Post a Comment