MIRADI yote ya barabara na madaraja ambayo Rais Jakaya Kikwete
ameahidi kuitekeleza, itafanyiwa kazi na kukamilishwa kwa wakati,
imeelezwa.
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, alisema hayo jana, akijibu swali
la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum-CHADEMA, Susan Kiwanga, aliyetaka
kujua ni lini ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ya kujenga barabara ya kutoka
Kidatu kwenda Morogoro itatekelezwa.
Akijibu, Dk Magufuli alisema kuwa, ahadi yoyote inayotolewa na Rais
katika eneo lolote nchini, kwa mawaziri wa Serikali hilo ni agizo na
watendaji wake watahakikisha zinatekelezwa.
Dk Magufuli alisema, ujenzi wa barabara hiyo utaanza pindi usanifu wa
kina utakapokamilika na baada ya kumalizika kwa ujenzi wa daraja la mto
Kilombero.
Akijibu swali la Mbunge wa Mpanda Vijijini, Moshi Kasoko, kuhusu
ujenzi wa barabara inayounganisha mkoa wa Kigoma na Katavi Waziri
Magufuli alisema Serikali imetenga Sh bilioni 751 ili kuanza utaratibu
wa ujenzi wa barabara hiyo.
Dk Magufuli pia alimhakikishia Mbunge wa Meatu (CHADEMA), Meshack
Opulukwa, kuwa serikali inajenga daraja la mto Sibiri na kwamba
mkandarasi alisimama kwa muda tu kusubiri mafuriko yapungue.
Kuhusu swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Mpanda Mjini, Said
Arf (CHADEMA), lini barabara ya lami kuunganisha wilaya ya Mpanda,
Mlela, Sikonge na Tabora, itajengwa Dk Magufuli alijibu kuwa upembuzi
yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara hiyo ya kilomita 364 kutoka
Mpanda kwenda Tabora umekamilika.
Alisema, “Serikali inakamilisha mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB), iliyokubali kutoa fedha za mkopo kwa ajili ya ujenzi wa
barabara ya Km 334, kwa kiwango cha lami, kutoka Mpanda hadi Pangale
(Tabora)”.
“Pia Serikali kwa kutumia fedha za ndani, imeanza kujenga sehemu ya Pangale–Tabora yenye urefu wa Km 30”
No comments:
Post a Comment