Magufuli: Barabara zetu hazivimbi

WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli amesema jana kuwa barabara zina vimba na kuharibika kwa sababu, zinakuwa zimefikisha muda wake wa mwisho wa matumizi zikiwa na ubora wake, ambao ni miaka 20.
Aidha, alisema kuwa, tofauti na nchi za bara la Ulaya zinazoruhusu usafirishaji wa mizigo kwa uzito wa kati, Tanzania inaruhusu magari ya mizigo ya tani hadi 100 kupita kwenye barabara zisizohimili vishindo, hivyo kuziharibu.
Waziri Magufuli alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa CUF, Hamad Rashid aliyetaka kujua sababu za kuvimba kwa barabara nyingi zilizo jengwa kwa kiwango cha lami, katika maeneo tofauti nchini, muda mfupi baada ya wakandarasi kuzikabidhi na kuanza kutumika.
Waziri alijibu, “Barabara zetu hazivimbi. Kinacho tokea ni kuwa zinaharibika kwa sababu muda wake wa matumizi zikiwa na ubora wake unakuwa umekwisha.
Kwa kawaida, ndani ya muda huo, barabara hupaswa kufanyiwa matengenezo kwa kuwa zinakuwa zikitumika”. Wakati huo huo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda, ametoa ufafanuzi kuhusu kanuni inayomtaka Waziri Mkuu, ajibu maswali ya papo hapo bungeni.
Spika alilazimika kutoa ufafanuzi huo, baada ya Mbunge wa ChakeChake, Mussa Haji Kombo kusimama na kuhoji sababu za Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoonekana bungeni mara nne mfululizo siku za Alhamisi kujibu maswali yao ya papo hapo.
“Wabunge ninawaomba muwe mnasoma kanuni za bunge na kuzielewa. Kanuni husika inasema kuwa, Waziri Mkuu atajibu maswali ya wabunge ya papo hapo endapo atakuwepo bungeni,” alisema Spika.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved