Kafulila ang’ang’ana mabehewa feki

MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR Mageuzi) ameitaka Serikali kuwasilisha bungeni taarifa ya kashfa ya ununuzi wa mabehewa feki katika Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kusababisha hasara ya Sh bilioni 230.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni jana, mbunge huyo alisimama kuomba muongoza wa Spika kwamba kutokana na unyeti wa jambo hilo, ikiwa ni pamoja na madai kwamba Kampuni iliyopewa zabuni ya kuagiza mabehewa hayo haikuwa na uwezo huo, kwa nini suala hilo lisipelekwe bungeni kujadiliwa.
Mbunge huyo alihoji kwamba si vyema suala hilo likazungumzwa na kuishia nje ya Bunge badala ya kujadiliwa na kupata ufumbuzi, lakini akijibu muongozo huo Spika wa Bunge, Anna Makinda alisema jambo hilo ni la kisekta na kwamba lilitakiwa lianzie kwenye kamati inayohusika.
Hata hivyo, akichangia muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 wenye lengo la kuzifanyia marekebisho sheria 16 zinazohusu masuala ya fedha, kodi, ushuru na tozo mbalimbali nchini uliowasilishwa jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, mbunge huyo alirudia suala hilo la TRL akisema kuna haja ya jambo hilo kufanyiwa kazi kwani matumizi mabovu ya sh bilioni 230 hayawezi kufumbiwa macho.
Alisisitiza taarifa ya jambo hilo ipelekwe bungeni na kuhoji kampuni hiyo iliyohusika na kuagiza zabuni hiyo imelipwaje fedha zote hizo kabla ya kutimiza masharti na kumuomba Spika Makinda aagize taarifa iwasilishwe bungeni na sio kuwalinda.
Kauli hiyo ya kuwalinda ilimfanya Spika Makinda kusimama na kusema halindi mtu na kumtaka mchangiaji ajielekeze katika hoja husika.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta wakati akifanya majumuisho ya bajeti yake Mei mwaka huu, alisema maofisa watano wa serikali wanatarajiwa kupandishwa kizimbani hivi karibuni, kutokana na kashfa ya uagizaji wa mabehewa 274 kutoka India, huku wengine wakitarajiwa kuchukuliwa hatua za kiutawala.
Aprili mwaka huu, Sitta alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Kipallo Kisamfu na wengine wanne, ili kupisha uchunguzi wa kashfa ya uingizaji wa mabehewa feki ya mizigo.
Wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Mitandao, Ngosomwile Ngosomiles, Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa, Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiranga na Meneja Mkuu wa Manunuzi, Ferdinand Soka.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved