Hatimaye Dk Migiro ajitosa kuwania urais

Hatimaye Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais baada ya kutajwa kwa muda mrefu kuwa na mipango ya kuomba kuingia Ikulu.
Migiro anakuwa mwanamke wa nne kuchukua fomu hizo baada ya Amina Salum Ali, Dk Mwele Malecela na Monica Mbega, na mwanachama 35 wa CCM kuingia kwenye mbio hizo za kuelekea Ikulu kwa tiketi ya chama tawala.
Kwa muda mrefu, Dk Migiro amekuwa akitajwa kama mtu ambaye anaweza kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, hasa kutokana na hoja ya “nafasi ya wanawake” kushika urais, lakini amekuwa hazungumzii suala hilo wala hakuwahi kutangaza nia.
Ubashiri huo ulizidi wakati alipomaliza mkataba wake Umoja wa Mataifa na kurejea nchini ambako aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa mbunge na baadaye kushika nafasi yake ya sasa.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu hizo, Dk Migiro, aliyesindikizwa na mumewe, Profesa Cleophas Migiro na mbunge wa viti maalum, Anne Abdallah, alisema anasubiri Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Msaidizi huyo wa zamani wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema ni imani yake kuwa Ilani hiyo kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 itakuwa imefanya tathimini katika maeneo yaliyopo katika ilani inayoisha.
“Na mimi nitaweka mikakati ya kuendeleza yale ambayo yameshafanyika. Sasa endapo nitapata ridhaa ya chama changu, nyenzo yangu kuu itakuwa ni Ilani ya Uchaguzi ya CCM,” alisema.
Alisema kwa kuwa uchumi umeendelea kukua awamu hadi awamu, na yeye atahakikisha kukua kwa uchumi kunawafikia wananchi wengi zaidi.
“Nitahakikisha kuwa mambo haya yaliyofanywa na awamu za uongozi zilizopita yanakuwa stahamilivu na endelevu na kuwafikia wananchi walio wengi zaidi,” alisema.
Alisema kwa atazingatia misingi iliyowekwa na awamu zilizopita, na kwamba mkazo utawekwa katika kilimo, viwanda, afya na miundombinu katika serikali ijayo.
Alisema kwa sababu ya ongezeko la watu, kilimo, viwanda na miundombinu, huduma za afya zinahitaji kuendelezwa ili ziendane na ongezeko hilo.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved