Wagombea hao jana waliendelea kusaka wadhamini
huku Makongoro Nyerere, akieleza kuwa kuna ugonjwa wa kuvunja kanuni na
Stephen Wasira akisema hakuna mafisadi ndani ya CCM wakati Dk Gharib
Mohamed Bilal na Samuel Sitta wakirejesha fomu.
Fomu hizo, ambazo wagombea 34 wamezijaza na
wanatakiwa kuzipeleka mikoa mbalimbali kutafuta wadhamini, ndizo
zitakazotumika kujadili makada hao na kuwachuja hadi kubakia wagombea
wasiozidi watano ambao watapelekwa Halmashauri Kuu na baadaye Mkutano
Mkuu kwa ajili ya kupigiwa kura kupata mwanachama atakayepeperusha
bendera ya CCM.
Kwa mujibu wa fomu hizo ambazo Mwananchi imepata
nakala zake, wagombea hao watatakiwa waeleze iwapo waliwahi kukihama
chama hicho kikongwe au ASP, kutaja jina la chama walichojiunga nacho na
kueleza walikaa huko kwa muda gani.
Wagombea watakaotakiwa kutoa maelezo kwenye
kipengele hicho ni mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira na mbunge wa
Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere.
Makada hao wawili waliihama CCM wakati wa uchaguzi
mkuu wa kwanza tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi nchini mwaka
1995, na kuhamia NCCR-Mageuzi na wote walishinda ubunge.
Hata hivyo, ubunge wa Makongoro ulitenguliwa na mahakama wakati Wasira alimaliza kipindi chake cha miaka mitano.
Hata hivyo, kigezo hicho ni sehemu tu ya maswali
yaliyowekwa kwenye fomu hiyo na itategemea jinsi watakavyojieleza
kukidhi Kamati Kuu ya CCM ambayo inaundwa na vigogo 34.
Vilevile fomu hizo zinawataka makada wanaoomba
kuteuliwa kuwania nafasi hiyo ya juu nchini, kueleza iwapo waliwahi
kuadhibiwa na chama au na jumuiya ya chama kwa kosa lolote.
Kipengele hiki kinaweza kuwabana wagombea sita
waliopewa onyo kali na Kamati Kuu kwa kuanza kampeni mapema na kuhusiana
na vitendo vinavyokiuka maadili.
Wagombea walioadhibiwa kwa kosa hilo ni Wasira na
mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye. Wengine ni
January Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Taknolojia, William Ngeleja (mbunge wa Sengerema) na Bernard Membe
(Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa).
Pia fomu hizo mbali na kuwataka wagombea kukusanya
wadhamini 450 katika mikoa 15, mitatu kati yake ikiwa ya Zanzibar,
zinamtaka kila mmoja kueleza iwapo aliwahi kupatikana na hatia
mahakamani ya kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali na kama aliwahi
kufanya hivyo, ataje kodi gani na alipewa adhabu gani.
No comments:
Post a Comment