SERIKALI imesema inatarajia kuanza kutumia bandari ya Tanga katika
kuingiza mafuta ili kupunguza msongamano na ucheleweshwaji wa upakuaji
katika bandari ya Dar es Salaam pamoja na kuongeza ufanisi wa
usafirishaji wa nishati hiyo.
Kuanza kutumika kwa bandari ya Tanga kunatarajiwa kuongeza ufanisi wa
usafirishaji wa mafuta, kupunguza ucheleweshwaji pamoja na kuongeza
usalama wa usafirishaji wa nishati hiyo muhimu.
Akizungumza katika Mkutano wa wadau wa mafuta nchini uliofanyika
jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma
za Nishati na Maji (EWURA), Felix Ngamlagosi alisema tangu waanze mfumo
mpya mwaka 2012 waliifunga bandari ya Tanga kupakua mafuta.
“Tulipoanzisha mfumo mpya wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja mwaka 2012
tulisitisha kuingiza mafuta katika bandari ya Tanga, na mfumo huo
umekuwa na mafanikio makubwa sana,” alisema Ngamlagosi.
Alisema kwa kuwa mfumo huo umekuwa na mafanikio makubwa, wameamua
kuifungua rasmi bandari ya Tanga ili ianze kutoa huduma ya kupakua
mafuta na kuwa mbadala wa bandari ya Dar es Salaam.
Kutumika kwa bandari hiyo kunatarajiwa kuongeza kasi ya maendeleo
katika mkoa wa Tanga, kuongeza upatikanaji wa ajira, kupunguza
msongamano wa meli katika bandari ya Dar es Salaam na pia kuwa mbadala
wa usafirishaji wa mizigo endapo kutatokea tatizo lolote katika bandari
ya Dar es Salaam itatumika ya Tanga.
No comments:
Post a Comment