Mbowe ahukumiwa mwaka mmoja

MAHAKAMA ya wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, imemtia hatiani na kumhukumu Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh milioni moja, kutokana na kesi iliyokuwa ikimkabili ya kumshambulia mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Akisoma hukumu hiyo iliyohudhuriwa na wabunge wengi wa Chadema, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Denis Mpelembwa, alisema mahakama imemkuta Mbowe na hatia, hivyo kutakiwa kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini kiasi cha Sh milioni moja.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai, katika kesi hiyo ya jinai namba 73 ya mwaka 2011, alidaiwa kumshambulia Nassir Yamin, katika Kijiji cha Nshara, kata ya Machame Kaskazini, Wilaya ya Hai, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Mpelembwa alisema mahakamani hapo kuwa hukumu iliyotolewa mahakamani hapo imezingatia ushahidi uliotolewa kwa upande wa mlalamikaji Nassir Yamini.
Kwa upande wake, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe akizungumza mahakamani hapo, alisema hukumu iliyosomwa mahakamani hapo haijamtendea haki.
Alisema kesi yake hiyo haikustahili kuchukua muda mrefu kama mahakama ilivyofanya kwa kuchukua zaidi ya miaka mitano bila kusomewa hukumu.
Hata hivyo, Mbowe amelipa kiasi cha fedha Sh milioni moja alichotakiwa kulipa kama hukumu ilivyoeleza, kwa kumtaka kulipa kiasi hicho cha fedha au kwenda jela mwaka mmoja.
Lema na Polisi
Wakati Mbowe akihukumiwa, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema jana alishindwa kuzuia hasira zake na kutaka kupigana na mmoja wa askari polisi katika kituo cha kuandikisha wapigakura cha Mkombozi kata ya Sokoni One, Jimbo la Arusha.
Tafrani hii ilitokea baada ya kukuta polisi huyo akiandikisha wananchi wanaohitaji vitambulisho, kabla ya kuingia ndani ya chumba cha waandikishaji.
Vurugu hizo zilitokea saa 5:30 asubuhi, mara baada ya Lema kuingia eneo hilo akitembelea vituo vya kuandikisha wapiga kura kuangalia hali halisi.
Alipofika kwenye kituo hicho alikuta mmoja wa Polisi akiwa amevaa kiraia (Jina halikupatikana mara moja), akiwa na daftari dogo akiorodhesha majina ya wapiga kura kwa lengo la kupunguza foleni.
Akizungumza na wananchi huku Lema akiwa amezungukwa na askari polisi, alisema huo sio utaratibu wa kufanywa na polisi na hata Tume hairuhusu Polisi kufanya kazi hiyo bali kulinda amani tu.
Hata hivyo, Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi cha Arusha, Thomas Maleko, akimtuliza hasira Lema akisema wao wanafanya kazi hiyo, ili kuwapunguzia adha wananchi ambao wanafika kituoni saa 9:00 usiku, hadi siku ya pili wanakaa kutwa nzima bila kupata fursa ya kuingia chumba cha kujiandikisha.
Alisema kutokana na hali hiyo, ndipo Polisi walipoamua kuandikisha watu kwa makubaliano na waandikishwaji wenyewe, ili waondoke nyumbani wakafanye kazi zingine na kesho yake wakirejea wanapata fursa hiyo.
“Hawa watu hata wakikaa hapa hawawezi kuingia ndani ya chumba husika, maana kuna kompyuta moja tu, hivyo wanapigwa na jua, hivyo utaratibu huu sisi tumeona ni mzuri, tunaandika jina la mtu kisha tunamruhusu aende nyumbani hadi kesho aje anaingia ili kupata kitambulisho,” alisema.
Hata hivyo, licha ya maelezo ya polisi, Lema hakukubaliana nayo na kuwasiliana na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Idd ambaye alimtuma Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi, ambaye naye hakutaka kuzungumza chochote na waandishi wa habari na pia hakutaka kutaja jina lake.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved