ALIYEKUWA Waziri wa nishati na madini kabla hajajiuzulu, Prof.
Sospeter Muhongo, amesema wawania urais wanaowaambia wananchi kuwa
watafufua viwanda vilivyokufa au kubinafsishwa kwa wawekezaji ambao
wamebadili matumizi ya majengo hayo, hawasemi ukweli.
Aliyasema hayo jana katika ofisi ya CCM Mbeya Mjini, alipokuwa
akizungumza na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliojitokeza
kumdhamini na kumsikiliza ili achaguliwe na chama hicho kuwania nafasi
ya urais mwaka huu.
“Anayeahidi kuwa atafufua hivi viwanda vikiwepo vya hapa Mbeya na kule
kwetu Mara ni mtu wa karne moja kurudi nyuma, maana viwanda hivi hata
viwanda vilivyotengeneza spare zake huko nje navyo havipo. Mimi
nitakachokifanya ni kujenga viwanda vipya vya kisasa” alisema huku
akishangiliwa.
Alisisitiza kuwa, wananchi wa Tanzania wa sasa, hawahitaji propaganda
bali wanahitaji kuoneshwa njia ya kutatua matatizo yao kwasababu
wamechoshwa na umasikini.
Aliwaambia wanachama hao kuwa Tanzania ina mali nyingi sana na
inahitaji kiongozi mwenye mawazo mapya na mbinu mpya za kutatua
umasikini ulio miongoni mwa jamii badala ya kuchagua viongozi wale wale
ambao wanaahidi yale yale yanayoshindwa kuwakwamua wananchi.
“Mimi siombi nafasi ya urais kwasababu nafasi ipo wazi na kutaka
kwenda na marafiki Ikulu, bali ninahitaji nafasi hii kwasababu ya
kuondoa umasikini kwa watanzania na mtaji katika nchi hii upo katika
madini na asilimia kama kumi pekee ya madini ndiyo yaliyochimbwa hapa
nchini” alisema Prof. Muhongo.
Alisema anajivunia katika usimamizi wa umeme kwa kipindi chake ambapo
Tanzania ina jumla ya Vijiji 15,186 na hadi kufikia mwaka 2012 ni vijiji
3, 734 sawa na asilimia 24.6 ndivyo vilikuwa na umeme. Miradi
iliyosimamiwa kwa umahiri wake ikiwemo kutafuta fedha kutoka nje ya nchi
na kufikisha Vijiji 5,234 Juni 2015 mwaka huu na umeme huo
unaunganishwa kwa Shilingi 27, 000 sawa na majogoo matatu ya kuku.
Kwa takwimu hizo, Mtandao Huu wa New Day Taarifa
umebaini kuwa katika suala la gharama za kuunganisha umeme kwa mkoa wa
Mbeya hasa Vijjini si kiasi hicho kilichotajwa na Prof. Muhongo, bali
kiasi kinachotozwa kwa ajili ya kuunganishiwa umeme ni Shilingi 177,000,
fedha ya mkandarasi anayetambulika na shirika hilo ni Shilingi
45,000-80,000/= na nauli ya kukodi Tax kwa injinia wa Tanesco kwenda
kuangalia nyumba ilipo kijijini ni Shilingi 10,000 – 20,000/=
Hata hivyo, Prof. Muhongo alipata wadhamini 45 ambapo baadhi ya
waliokuwa wamejitokeza kwa ajili ya kumdhamini hawakupata nafasi ya
kufanya hivyo akiwemo Mchungaji Anyelwisye Mwaisela kutoka Mbalizi
wilaya ya Mbeya Vijijini ambapo aliwaomba wajitokeze kumdhamini katika
uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba mwaka huu.
Wawania wengine nafasi ya urais kupitia chama hicho ambao wanatarajia
kudhaminiwa na wanachama wa mkoa wa Mbeya ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu,
Edward Lowassa ambaye anatarajia kufika mkoani Mbeya Juni 19 mwaka huu
na Prof. Mark Mwandosya anayetarajia kufika Juni 22, mwaka huu huku
duru za siasa zikisema kuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Rungwe Ally
Mwakalindile, anakotoka Prof. Mwandosya, amejiunga rasmi kambi ya
Lowassa na alitambulishwa rasmi katika kikao kilichoketi katika Hotel ya
Beaco Jijini Mbeya Jumapili ya Juni 14, mwakahuu kikiongozwa na
Mwenyekiti wa Mbeya Mjini ndugu Mwaitenda.
No comments:
Post a Comment