SERIKALI imeshauriwa kujizatiti katika kulinda viwanda vya ndani kwa kuzuia uingizwaji wa saruji na sukari kutoka nje ya nchi.
Aidha, Serikali imetakiwa kujielekeza zaidi katika kukusanya kodi
kwenye sekta ya mawasiliano hususani katika matumizi ya simu za mkononi.
Akichangia katika mjadala wa Bajeti Kuu ya serikali unaondelea
bungeni mjini hapa, Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM) alisema sukari
kutoka nje ya nchi imekuwa ikiingizwa kwa wingi kinyemela, jambo ambalo
linadhoofisha viwanda vya ndani.
“Nipongeze hatua ya Serikali kuweka kodi katika uingizwaji wa sukari
inayotoka nje katika bajeti ya mwaka huu, kwani itasaidia kudhibiti
uingizaji holela wa sukari unaochangia kuua viwanda na kuongeza mapato
ya serikali,” alisema.
Pia aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kudhibiti uingizwaji wa
saruji kutoka nje ambao hivi sasa umekithiri na kuathiri viwanda vya
ndani ya nchi.
Naye Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF), alisema bidhaa
zinazoingia kinyemela kutoka nje ya nchi zipo nyingi ikiwemo saruji na
sukari hali hiyo inaua viwanda vya ndani, wamiliki na wafanyakazi wa
viwanda hivyo.
Kuhusu ukusanyaji wa kodi, Khalifa aliishauri Serikali kuwa na vyanzo
vipya vya mapato kwa kujikita katika kukusanya mapato ya simu ambayo
amesema serikali inaweza kupata fedha nyingi.
Mbunge wa Kwela, Ignas Malocha (CCM) alisema kutofikiwa kwa malengo
ya makusanyo ya kodi kunatokana na tatizo la uaminifu kwa baadhi ya
watendaji.
Alizungumzia kitendo cha serikali kutowalipa wakulima madeni yao kwa
takribani miezi nane sasa. Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia ametaka
ushirikishwaji wa binafsi kwenye uchumi na kutaka uimarishwaji wa
bandari ili uweze kusaidia kuongeza mapato.
No comments:
Post a Comment